Abstract:
IKISIRI
Utafiti huu umeshughulikia mwelekeo wa kiubwege katika tamthilia ya Kiswahili,
mintarafu ya Amezidi (1995) na Beluwa (2012). Nadharia iliyoongoza kazi hii ni
nadharia ya Ubwege iliyoasisiwa na Albert Camus ambayo, kimsingi imeangazia
ukosefu wa maana ya maisha ya binadamu ulimweguni. Data za uchunguzi huu
zilitokana na uhakiki wa kazi hizi mbili kwa misingi ya mihimili ya nadharia ya
ubwege. Madhumuni ya utafiti huu ni pamoja na; kuchunguza vipengele vya
kiubwege kimaudhui na kifani katika tamthilia ya Amezidi na Beluwa, kujadili
mwelekeo wa kiubwege katika tamthilia ya Amezidi na Beluwa pamoja na kutathmini
mwelekeo wa kiubwege katika The Myth of Sisyphus. Kutokana na madhumuni haya,
utafiti huu umejiegemeza kwenye nadharia tete kwamba Beluwa na Amezidi ni
tamthilia za kiubwege, kuna kufanana kwa mwelekeo wa kiubwege katika tamthilia
ya Amezidi na Beluwa na Albert Camus aliweka msingi wa nadharia ya Ubwege
katika The Myth of Sisyphus . Tofauti na tafiti zilizofanywa hapo awali, utafiti huu
umejikita katika mwelekeo wa kinadharia ambao wahakiki wengi hawakuzingatia
katika tamthilia ya Amezidi. Aidha, utafiti huu umehusisha ulinganifu kinadharia
ambao haukuchunguzwa na wahakiki wa awali. Huu ni utafiti wa kiuhakiki, na hivyo
mbinu zilizotumiwa kukusanya data ni utafiti maktabani ambapo usomaji makinifu
wa tamthilia hizi mbili ulichangia katika kudondoa vipengele vya kiubwege kama
vinavyojitokeza katika tamthilia hizi mbili, na kudhihirisha mwelekeo wa kiubwege
wa watunzi hawa pamoja na kubainisha mwelekeo wa kiubwege katika The Myth of
Sisyphus (1942). Maktaba tuliyotumia ni ya Margaret Thatcher ya Chuo kikuu cha
Moi, ambamo tulisoma majarida, vitabu na makala zinazohusiana na mada ya utafiti.
Kadhalika tulitembelea tovuti mbalimbali zinazozungumzia Ubwege pamoja na
kupakua makala mbalimbali yanayohusu ubwege. Mbinu ya kitaamuli ilitumika
katika uchanganuzi wa data tuliyokusanya na kueleza matokeo ya utafiti. Matokeo ya
utafiti huu yalionyesha kwamba tamthilia ya Amezidi na Beluwa ni kazi za kiubwege
na watunzi walifuata mwelekeo wa kiubwege wake Albert Camus; ambaye anashikilia
kwamba Mungu yupo japo binadamu hapaswi kuishi kwa matumaini ya
kukombolewa naye bali, afanye juhudi za kujipatia maana ya maisha yake akisubiri
kifo-ambacho ndicho hatima ya binadamu wa kiubwege. Mbali na utafiti huu kuweka
wazi mwelekeo wa kiubwege wa Albert Camus katika The Myth of Sisyphus (1942),
utaongeza maarifa yaliyopo kuhusu tamthilia za kiubwege na fasihi kwa jumla.