Abstract:
Riwaya za Kiswahili zilizoandikwa katika miaka ya hivi karibuni zinakaidi uandishi
uliozoeleka wa kimapokeo uliopendekezwa na akina Aristotle, na kugeukia mtindo
mpya wa uandishi wa kimajaribio wa kibaadausasa. Utafiti huu basi unachunguza
uandishi wa kibaadausasa katika riwaya zilizoteuliwa za Kiswahili zilizoandikwa
katika K21, yaani, Dunia Yao, Nyuso za Mwanamke na Unaitwa Nani? Riwaya hizi
zina matumizi mengi ya uhalisia mazingaombwe ambayo huenda kinyume na kaida za
uhalisia. Licha ya hayo, waandishi wa riwaya hizi hurejelea matini nyingine katika kazi
zao zikiwemo za kifasihi, kidini, kisanaa, kihistoria, kifalsafa na kisaikolojia. Hata
hivyo, uandishi huu mpya haujafanyiwa utafiti wa kutosha ili kuubainisha katika
maandishi ya fasihi ya Kiswahili na kuonyesha athari zake kwa msomaji wa kazi hizi.
Lengo la utafiti lilikuwa ni kubainisha na kuhakiki vipengele vya ubaadausasa katika
riwaya zilizotafitiwa kama vile matumizi ya uchopekaji wa vipande vya simulizi,
matumizi ya uhalisia mazingaombwe na matumizi ya mwingiliano matini. Utafiti huu
uliegemea katika falsafa ya ubaadausasa na kuongozwa na nadharia ya ubaadausasa
ambayo hupendekeza uanuwai wa mawazo kwa kukaidi kuwepo na mtazamo mmoja
wa kueleza ulimwengu na tajriba za binadamu, au simulizi kuu. Usampuli wa
kimaksudi ulitumika kupata data kwa kujikita katika riwaya zilizoandikwa katika K21
na ambazo zilidhihirisha vipengele vya ubaadausasa. Data ilikusanywa kupitia usomaji
wa kina wa riwaya zilizoteuliwa kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya ubaadausasa
iliyodhihirika kwa wingi katika riwaya hizo. Data ilichanganuliwa kwa kutumia
mihimili ya nadharia ya ubaadausasa na kuwasilishwa kwa lugha ya nathari. Utafiti
uligundua kuwa baadhi ya vipengele vya kibaadausasa vilitumiwa kimaksudi na
waandishi ili kukaidi simulizi kuu zilizotawala. Riwaya za kibaadausasa zilitumia
uchopekaji wa vipande vya simulizi kuvuruga urazini, mshikamano na muumano wa
usimulizi wa riwaya za kimapokeo. Kimaudhui, riwaya hizi zinapuuza na kutilia shaka
simulizi kuu inayohusiana na maana ya uhuru katika mataifa mengi ya Afrika kwa
kusaili mwelekeo chanya uliohusishwa uhuru kuwa ungeleta maendeleo katika mataifa
na badala yake kuonyesha hali ya utamauishi inayotawala mataifa haya. Riwaya hizi
pia zinasaili hali ya utumwa miongoni mwa Waafrika wanaohamia ughaibuni kutafuta
maisha bora humo kwa kuonyesha changamoto ambazo wahamiaji hupitia. Hali
kadhalika, riwaya hizi zinafichua itikadi zilizofichika ndani ya misaada inayoletwa
katika mataifa ya Afrika kutoka mataifa ya Ulaya na kuibainisha kama chambo cha
kueneza ukoloni mamboleo kwa urahisi katika K21. Hali kadhalika, katika riwaya
zilizotafitiwa mipaka kati ya uhalisia na umazingaombwe imezibwa kupitia matumizi
ya wahusika na matukio ya ajabu kama vile mizuka, vivuli, wafu pamoja na wahusika
wenye nguvu za kiajabu ili kuwakilisha hali halisi ya dunia ya sasa ambayo imejaa
mambo mengine ya ajabu yasiyoelezeka. Fauka ya hayo, utafiti uligundua kuwa riwaya
zilizoteuliwa zilitumia mwingiliano matini kwa wingi. Kutokana na matokeo ya utafiti
huu, tunahitimisha kwa kusema kuwa mtindo wa uandishi wa ubaadausasa umetumika
sio tu kama mbinu ya kiumbuji bali katika kudhihirisha fujo, ghasia na ukosefu wa
mshikamano katika ulimwengu wa K21 kwa kukaidi simulizi za awali. Utafiti huu
unatoa mchango katika taaluma ya usomi kwa kueleza vipengele vya ubaadausasa
katika riwaya zilizoteuliwa za utafiti huu na namna ya kuzisoma kwa jumla.