Abstract:
Licha ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na habari bado turathi za kifasihi simulizi
zikiwemo nyimbo zingali zinaheshimiwa na jamii nyingi za Kiafrika kwa kuwa ni
tunu inayotumika kuhifadhi historia, kuendeleza amali za jamii na pia ni chemchemi
ya burudani. Kutokana na umuhimu wa nyimbo katika jamii, utafiti huu umechunguza
utendaji wa nyimbo za mdumange kutoka jamii ya Wasambaa wa Lushoto, Tanga –
Tanzania kwa minajili ya kutathmini nafasi ya utendaji wa nyimbo za mdumange
katika mwonoulimwengu wa Wasambaa. Madhumuni mahsusi ya utafiti huu
yalikuwa: (i) Kupambanua jinsi miktadha ya kijamii inavyochochea utendaji wa
nyimbo za mdumange; (ii) Kuchanganua usawiri wa maisha ya Wasambaa kupitia
mitindo ya lugha inayotumika katika nyimbo za mdumange na; (iii) Kujadili nafasi ya
mitindo ya viziada lugha kwa wasanii wa nyimbo za mdumange na jamii ya
Wasambaa kwa ujumla. Data zilikusanywa nyanjani kwa kutumia mikakati ya
uchunguzi shiriki, usaili na mijadala ya vikundi. Vifaa vilivyotumika vilikuwa
kamera, kinasa sauti na redio kaseti. Uchambuzi wa data uliongozwa na Nadharia za
Utendaji wa Maigizo pamoja na Semiotiki ya Kijamii. Kulingana na Nadharia ya
Utendaji wa Maigizo, utendaji ni tukio la aina yoyote ile linalowajumuisha hadhira
pamoja na fanani wake kwa minajili ya kuigiza au kuonyesha tabia za wanadamu.
Nadharia hii ilichaguliwa kwa kuwa katika jamii nyingi za Kiafrika utendaji ni
mojawapo ya kanuni za maisha ya kila siku. Kutokana na mihimili ya Nadharia hii,
utendaji unachukuliwa kuwa ndicho kiungo cha fasihi simulizi chenye uwezo wa
kudhihirisha ujumi na diskosi za wanajamii. Kwa upande mwingine, Nadharia ya
Semiotiki ya Kijamii ilitumika kwa minajili ya kupambanua misimbo au ishara
zinazohusika wakati wa utendaji. Wafuasi wa Nadharia hii wanaeleza kuwa Semiotiki
huchunguza maana katika ishara pamoja na kuonyesha uhusiano kati ya ishara husika
na mifumo mbalimbali ya jamii. Kimsingi, kupitia utafiti huu imegundulika kuwa
nyimbo za mdumange ni sanaa thabiti ya Wasambaa iliyosheheni vipashio mbalimbali
vya ujumi, hususan lugha na viziada lugha. Kadhalika, kupitia utafiti huu
imedhihirishwa kuwa utendaji wa fanani na hadhira unaimarishwa na mitindo ya
lugha na viziada lugha. Kwa kutumia mitindo hiyo, fanani na hadhira wanajadili
itikadi mbalimbali za maisha ya Wasambaa kijamii, kisiasa, na kiuchumi. Kwa
ujumla, utafiti huu umegundua kuwa utendaji wa nyimbo za mdumange umekuwa
ukichochewa na miktadha anuai ya Wasambaa kama vile turathi simulizi,
mwingiliano na jamii nyingine pamoja na mfumo wa maisha ya Wasambaa
unaodhihirika kwenye sherehe za harusi, dini na siasa. Imegundulika pia kuwa
utendaji wa nyimbo za mdumange una nafasi kubwa katika jamii ya sasa ya
Wasambaa. Nyimbo hizo hutumika kwa minajili ya kuburudisha, kuelimisha,
kuhifadhi turathi na kufasiri mwonoulimwengu wa Wasambaa. Pamoja na matokeo
haya, utafiti huu umependekeza kuwa ipo haja ya kuchunguza utendaji wa nyimbo
nyingine za jamii, hususan nyimbo za maombolezo