Abstract:
Utafiti huu umehusisha uchunguzi wa usuli wa sanaa ya tafsiri. Utafiti umechanganua
kipengele cha ukiushi katika tamthilia Nitaolewa Nikipenda ambayo ni tafsiri ya Kiswahili
ya tamthilia Ngaahika Ndeenda. Utafiti huu umefanya uchanganuzi linganishi wa lugha
iliyotumiwa katika Matini Chanzi ya Ngaahika Ndeenda iliyo katika lugha ya Gĩkũyũ na
Matini Tafsiri ya Nitaolewa Nikipenda iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Utafiti
umelenga kuchunguza Matini Tafsiri ilivyokiuka kutoka Matini Chanzi. Utafiti
umechunguza zaidi dhana kuwa Matini Tafsiri ni ‘kivuli tu’ cha Matini Chanzi na hivyo
kuihukumu kama kazi sahihi au isiyo sahihi. Utafiti huu umetumia Nadharia ya
Mawasiliano katika Tafsiri ya Nida ambayo ni nguzo ya kanuni na michakato muhimu
katika zoezi la tafsiri. Vitabu vya wataalamu mbalimbali vinavyohusu Nadharia ya Tafsiri
na ukiushi katika tafsiri vimesomwa na mawazo yao kunakiliwa. Ngaahika Ndeenda na
Nitaolewa Nikipenda vimesomwa kwa makini na kulinganishwa kwa mujibu wa lugha
iliyotumiwa kwa kutumia maana kama kaida. Utafiti huu umechanganua ukiushi katika
Tamthilia Tafsiri ya Nitaolewa Nikipenda na vilevile kujadili aina za ukiushi katika
Tamthilia hii. Aidha umbuji kama kiungo cha ukiushi katika Matini Tafsiri ulitathminiwa.
Tasnifu hii umejikita katika Nadharia ya Mawasiliano katika Tafsiri ya Nida ambayo
husisitiza mawasiliano mwafaka kati ya Matini Tafsiri na Hadhira Pokezi. Utafiti
umefanywa kwa kuchambua vitabu vya wananadharia wa tafsiri mbali na kuchanganua
maneno ya Matini Tafsiri kwa kuyalinganisha na maneno ya Matini Chanzi. Sampuli za
maneno, sentensi na vishazi vimetambuliwa na kunakililiwa kwa utaratibu, kuonyesha
vilivyowakilishwa katika Matini Chanzi ya Gĩkũyũ na chini yake vilivyohawilishwa katika
Matini Tafsiri ya Kiswahili. Maneno, vishazi na sentensi hizi zimechanganuliwa
kiulinganishi halafu mahitimisho kufanywa. Uchanganuzi wa data iliyoshughulikiwa
umethibitisha kuweko kwa ukiushi katika Matini Tafsiri. Ukiushi wowote uliopatikana
katika Matini Tafsiri umeainishwa katika aina mbalimbali za ukiushi mathalani ukiushi wa
kifonolojia, ukiushi wa kisintaksia na ukiushi wa kisemantiki. Athari ya maana ya ujumbe
katika Matini Chanzi na Matini Pokezi imechunguzwa pia. Utafiti umezingatia dhima ya
mtafsiri kama msanii na jinsi anavyokiuka maana iliyoko katika Matini Chanzi wakati
anapotafsiri. Ni matumaini yangu kuwa utafiti huu utawafaa wanafunzi na wasomi ambao
watatafitia mbinu za tafsiri katika kazi za kifasihi.