dc.description.abstract |
Kila lugha ni mfumo huru unaojitosheleza kisarufi. Ingawa hivyo, wasemaji wa lugha
tofauti wanapotagusana kimawasiliano, lugha zao huweza kuathiriana kisarufi, na athari
mojawapo huwa ni ukopaji wa msamiati. Ni kutokana na hali hii ambapo utafiti huu
ulichunguza kanuni zinazofuatwa katika uingizwaji wa msamiati mkopo wa Kiswahili na
Kiingereza katika Kikipsigis. Makala hii ilichunguza mabadiliko ya kimofofonemiki
yanayotokea katika msamiati mkopo unapoingizwa katika mfumo wa Kikipsigis.
Vilevile, sababu za ukopaji zilibainishwa. Data ya utafiti iliteuliwa kimakusudi. Utafiti
ulitambua kuwa Kikipsigis hufupisha irabu ndefu katika msamiati mkopo. Vilevile, irabu
unganifu husahilishwa ili zikubalike katika Kikipsigis. Kimsingi tulitambua kuwa
Kikipsigis hutohoa irabu ngeni kwa kutumia irabu asili zinazokaribiana kimatamshi.
Ilibainika pia kwamba Kikipsigis hakiruhusu mfuatano wa konsonanti mwanzoni mwa
neno. Kwa hivyo, Kikipsigis hutohoa msamiati wa aina hii kwa kuchopeka irabu. Katika
kuchunguza vichocheo vya ukopaji, makala hii ilibainisha kwamba Kikipsigis hukopa
msamiati ili kurejelea dhana ngeni isiyokuwepo katika utamaduni wake. Hata hivyo,
uchanganuzi ulionyesha kuwa Kikipsigis wakati mwingine hukopa msamiati hata kama
kina msamiati asilia kwa sababu ya ubadilishaji msimbo, msamiati mkopo ni sahili na
rahisi kutamkwa ukilinganishwa na kisawe chake cha Kikipsigis. |
en_US |