dc.description.abstract |
Matumizi ya lugha za kiasili yameshutumiwa na watu wengi kwa kukuza ukabila haswa
nchini Kenya. Hata hivyo, lugha hizi zinaweza kuwa rasilimali kwa wazungumzaji
zikitumiwa vyema. Utafiti huu ulilenga kuchunguza lugha za kiasili zinavyojitokeza kama
rasilimali kwa wazungumzaji wake zinapotumika katika redio za FM. Aidha, utafiti ulinuia
kujadili jinsi matumizi ya lugha za kiasili katika redio za FM yanavyowezesha jamii husika
kupata habari zinazoziwezesha kuboresha hali zao za maisha kwa njia mbalimbali. Uchunguzi
ulidhamiria hususan: Kuhakiki yaliyomo katika vipindi vya jamii, uchumi, siasa na afya
vinavyowasilishwa kwa kutumia Kibukusu katika redio za FM, zinazosikika katika kaunti ya
Bungoma; Kutathmini Kibukusu kinavyojitokeza kama rasilimali kuangazia masuala ya
jamii, uchumi, siasa na afya kwa wazungumzaji wake kinapotumika katika redio za FM, kisha
kutambua changamoto za matumizi ya Kibukusu kama rasilimali kwa wakaazi wa Bungoma
kupitia vituo vya redio za FM. Utafiti ulitumia mbinu za ustahilivu na kikiasi. Lahaja ya
Kibukusu ilitafitiwa katika mazingira halisi ambapo lugha hiyo hutumika na wazungumzaji
wake. Miktadha ya matumizi ya Kibukusu ilichunguzwa, hususan kama rasilimali kwa
wazungumzaji wake. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili; Sarufi Amilifu ya Halliday na
ya Uanzilishi wa Ajenda iliyoasisiwa na McCombs na Show. Sarufi Amilifu ilihusishwa
katika uchanganuzi wa vipindi vinavyopeperushwa kwa kutumia lugha za kiasili. Nadharia ya
Uanzilishi wa Ajenda ilitumika kuhakiki uteuzi wa vipindi vinavyopeperushwa na vituo hivyo
viwili vya redio. Uchunguzi ulifanywa katika vituo vya Sulwe na West FM vinavyopeperusha
matangazo kwa Kibukusu katika kaunti ya Bungoma. Utafiti ulihusisha mhariri mmoja,
watangazaji wawili na wataalamu wanne; mmoja kwa kila mojawapo ya masuala haya; jamii,
uchumi, afya na siasa ambao hualikwa kwa kila mojawapo ya vituo hivyo. Vilevile,
wasikilizaji 70 kutoka kila mojawapo ya vituo hivyo viwili vya redio walihusishwa. Kwa
jumla, utafiti uliwahusisha watu 154. Wasikilizaji hao waliteuliwa kutoka kwa kaunti ndogo
sita za kaunti ya Bungoma na walihusisha jinsia zote. Wasikilizaji waliteuliwa kwa kutumia
usampulishaji kimakusudi ambao huwezesha idadi ya wahojiwa kuongezeka kadiri utafiti
unavyoendelea. Vipindi vya redio vya vituo vyote viwili vilivyohusiana na masuala ya jamii,
afya, uchumi na siasa vilisikilizwa. Mbinu ya ujazaji wa hojaji kwa watangazaji na
wasikilizaji, usaili wa wahariri, watangazaji na wataalamu na kurekodi vipindi mahususi
zilitumika. Vifaa vifuatavyo vilitumiwa kukusanya data: hojaji kwa wanahabari, hohaji kwa
wasikilizaji, mwongozo wa usaili kwa wahariri, watangazaji na wataalamu na kinasa sauti
kunasia vipindi vilivyoteuliwa kisha vikachanganuliwa kwa kutumia nadharia ya Sarufi
Amilifu. Data ifuatayo ilikusanywa: vipindi vya redio vinavyotumia lahaja ya Kibukusu,
yaliyomo katika vipindi hivyo, Kibukusu kinavyojitokeza kama rasilimali kwa wazungumzaji
wake na changamoto za matumizi ya lahaja hiyo katika redio za FM. Data iliyokusanywa
ilichanganuliwa kwa kutumia maudhui yaliyomo kisha matokeo yakawasilishwa kwa maelezo
na takwimu. Matokeo ya utafiti huu yalikuwa yafuatayo: Matumizi ya lugha za kiasili katika
redio za FM yalijaza pengo liliokuwepo katika upashaji habari kwa watu walioko mashinani;
Matumizi ya lugha za kiasili katika redio za FM yaliwezesha wazungumzaji kufikia maamuzi
faafu kuhusiana na masuala ya afya, siasa, uchumi na jamii; ukosefu wa taasisi ya kudhibiti
uundaji wa istilahi ni mojawapo ya changamoto zinazokumba matumizi ya lugha za kiasili
katika redio za FM. Matokeo ya utafiti huu yalitoa picha halisi ya mchango wa lugha za
kiasili katika redio za FM nchini Kenya kwa maendeleo ya jamii husika. Matokeo ya
uchunguzi huu yatakuwa mchango kwa tafiti ambazo zimefanywa kuhusu matumizi ya lugha
za Kiafrika katika vyombo vya habari. Utafiti huu vilevile utawafaidi wapangaji lugha kitaifa
na katika viwango vya kaunti. Utafiti huu pia unatarajiwa kutoa mchango kwa uhifadhi na
makuzi ya lugha za Kiafrika kichanya. Utafiti unapendekeza yafuatayo: Kuundwa kwa taasisi
za kutafiti, kuunda na kudhibiti istilahi zinazotumika katika lugha za kiasili; Vyuo vikuu
kufundisha baadhi ya lugha hizi za kiasili ili kubadilisha mtazamo hasi kuzihusu; Serikali za
kaunti kuanzisha sera za lugha katika viwango vya kaunti na hatimaye, kufufuliwa kwa
ufundishaji wa lugha za kiasili mbali na Kiingereza, Kiswahili na lugha zingine za kigeni
kama vile Kifaransa na Kijerumani katika sera ya lugha nchini Kenya. |
en_US |