Abstract:
Istilahi mawasiliano ni tafsiri ya neno la Kiingereza „Communication‟ ambalo lina
asili ya Kilatini „Com-uni-care‟ linalomaanisha kujadiliana au kuwa na mazungumzo.
Mawasiliano ni mchakato ambao kwao habari hupokezwa baina ya mtu na mtu
kupitia kwa mfumo ulio sawa wa alama au matamshi au ishara. Mara nyingi,
mawasiliano haya huzua hisia kama furaha, huzuni, mapenzi na matumaini. Nyenzo
mojawapo ya mawasiliano miongoni mwa wapwani wa Kenya ni kupitia kwa Kanga.
Kanga ni kitambaa kipana chenye urefu wa sentimita 150 na upana wa sentimita 110
ambacho kwa kawaida huwa na maandishi ambayo hutumiwa kuwasilisha ujumbe
fulani. Kanga hununuliwa na kuvaliwa mbili mbili (gora). Utafiti huu unafafanua
uamilifu wa Kanga miongoni mwa wapwani wa Kenya kwa kuchunguza vazi hili
kama makala maalum ya kusomeka. Utafiti wetu umeongozwa na nadharia mbili:
Nadharia ya simiotiki iliyoasisiwa na Ferdinand de Saussure (1857 -1913), Charles
Pierce (1839 -1914) na Roland Barthes (1915 - 1980) wanaosisitiza kuwa kila ishara
huwakilisha ujumbe fulani. Nadharia ya uamali inayosisitiza kuwa muktadha ni
kipengele muhimu katika mawasiliano. Tumeibua data kwa kushirikiana na
wanajamii katika shughuli zao za kila siku huku tukiwasaili kuhusu Kanga na
matumizi yake. Aidha, tumewatembelea wauzaji na watengenezaji Kanga ili
watupatie data kuhusu mikondo inayotumiwa na wanunuzi wa kanga. Isitoshe,
tumesoma maandishi ya wasomi tofauti hasa yale yanayohusiana na mada yetu. Mbali
na hayo, tumepata ushauri kutoka kwa wataalam waliofanya utafiti kuhusu kanga
wakiwemo Sheikh Nabhany (shairi „Utendi wa Ulimwengu wa Kanga‟) Marie Beck
(Ambiguous Communication, kanga/leso) na Clarrisa Vierke. Mawasiliano yetu
yalikuwa ya njia ya simu, intaneti na ana kwa ana. Sampuli iliyotumiwa imeteuliwa
bila utaratibu maalum. Sura ya kwanza inatoa utangulizi wa tasnifu hii ilhali sura ya
pili inaelezea historia na dhima zingine za kanga. Sura ya tatu inafafanua mawasiliano
kupitia kwa kanga huku sura ya nne ikijikita katika kuchunguza uhusiano baina ya
muktadha mnamotokea mawasiliano na mawasiliano mahsusi. Sura ya tano
inatamatisha utafiti huu kwa kutoa mapendekezo.