Abstract:
Katika kusoma riwaya ya Caitaani Mutharaba-ini iliyoandikwa na Ngũgĩ wa Thiong’o
na tafsiri yake kwa Kiswahili, Shetani Msalabani na kwa Kiingereza, Devil on the
Cross, inabainika kwamba kuna tofauti zinazojitokeza katika jinsi ujumbe umesimbwa
na kuwasilishwa. Kando na kwamba tafsiri iliyotekelezwa imekiuka ubia wa
kimapokeo katika utekelezaji na uhawilishaji wa maana, matini za Kiswahili na za
Kiingereza zilizoangaziwa ni mazao ya tafsiri binafsi. Kwa jinsi hii, utafiti huu kwanza
ulichanganua udhihirikaji wa utamaduni, itikadi na utambulisho katika riwaya ya
Caitaani Mutharaba-ini. Utafiti aidha uliangazia jinsi dhana hizi zilishughulikiwa
katika tafsiri za Shetani Msalabani na Devil on the Cross. Uchanganuzi uliangazia
lugha hasa uteuzi wa kiisimu, vipengele vya fasihi simulizi na matumizi ya dhana
zinazofungamana na utamaduni chanzi. Utafiti huu vilevile ulichunguza namna itikadi
ilidhihirika kupitia kwa lugha katika riwaya hii na jinsi dhana hii ilihawilishwa katika
tafsiri za Kiswahili na Kiingereza. Dhana ya utambulisho ilishughulikiwa kwa
kuchunguza jinsi ilivyobainishwa katika Caitaani Mutharaba-ini na ilivyotafsiriwa
kwa Kiswahili na Kiingereza. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili: nadharia ya
Baadaukoloni katika tafsiri na nadharia ya Uchanganuzi wa Diskosi. Data ya utafiti
ilikusanywa kwa kutumia usampulishaji wa kimakusudi ambapo usomaji hakikifu
ulitekelezwa kwa matini husika kuambatana na azma na upeo wa utafiti huu. Data
ilipangwa kwa utaratibu wa vigeu vilivyokuwa vikijadiliwa na uchanganuzi
ukafanywa kwa njia ya maelezo. Uchanganuzi ulidhihirisha matumizi ya vipera vya
fasihi simulizi pamoja na dhana zinazofungamana na utamaduni chanzi katika kuumba
matini chanzi. Hali hii ilihusishwa na uteuzi wa kimakusudi ambao unabainika katika
fasihi ya baadaukoloni. Katika kuchunguza tafsiri, ilibainika kuwa mtafsiri
alichanganya baina ya mbinu ya uibuaji ugeni na ile ya ubinafsishaji katika
kuhawilisha dhana hizi za kitamaduni. Aidha, uteuzi wa kiisimu aliofanya mtafsiri
katika tafsiri ya Kiswahili na ile ya Kiingereza pakubwa ulibainishwa kuwa ulikuwa
wa kimakusudi na uliongozwa na msukumo wa kiitikadi. Utambulisho ulibainishwa
kuwa dhana ya kimsingi katika fasihi ya baadaukoloni na tafsiri yake ambapo mtafsiri
anatumia lugha kwa njia ya kimakusudi kuumba utambulisho maalum na kuuhawilisha
kadri ya dhima ya tafsiri yake. Kutokana na utafiti huu, ilidhihirishwa kwamba, tafsiri
aghalabu ni mchakato changamano wa mawasiliano. Vilevile, tafsiri ni jukwaa ambapo
mahusiano ya kiuwezo baina ya lugha na tamaduni tofauti hudhihirika. Hitimisho la
utafiti ni kwamba lugha katika tafsiri za baadaukoloni hutumiwa makusudi kwa lengo
la kukinza ubabe wa lugha na tamaduni za kibepari huku ikikweza tamaduni na lugha
za waliowahi kutawaliwa. Utafiti huu umependekeza haja ya kitaaluma ya kutambua
nafasi ya mtafsiri na athari yake katika mchakato wa tafsiri. Aidha, pana haja ya kutalii
dhana ya itikadi kama kipengele cha kimsingi katika utekelezaji na katika taaluma ya
tafsiri. Isitoshe, utafiti unapendekeza kwamba ni muhimu kuimarisha mwelekeo wa
nadharia ya baadaukoloni katika tafsiri kwa kujumuisha ndani mwake vipengele vya
uchanganuzi wa diskosi ili kuwezesha uchanganuzi wa kina. Mwisho, pana haja ya
kuzidi kupanua upeo wa utafiti katika taaluma ya tafsiri kwa Kiswahili kwa
kuchunguza vipengele zaidi vya ulinganifu katika tafsiri na ubora wa tafsiri.