Abstract:
Azma ya kutumia mifumo ya kielektroniki katika huduma za afya, inayojulikana kama
huduma za afya kielekroniki, ni kuboresha kiwango na upatikanaji wa huduma za afya
kwa wagonjwa. Aina mojawapo ya huduma za afya kielektroniki ni programu za afya
za rununu ambayo kwayo wagonjwa wanaweza kupokea huduma za afya kupitia simu
za rununu kwa usaidizi wa programu za mtandao. Kenya imeshuhudia ukuaji mkubwa
wa mpenyo wa kiteknolojia katika utoaji wa huduma za afya na ukuaji huu umeibua
suala la uteuzi na matumizi ya lugha za kiasili katika programu hizi za kielektroniki.
Kuambatana na haya, utafiti huu ulilenga kuchunguza nafasi na kiwango cha
ukubalikaji wa matumizi ya Kiswahili katika muktadha wa huduma za afya
kielektroniki nchini Kenya. Kwa hivyo, azma ya utafiti huu ilikuwa ni kutathmnini
upatikanaji na mpenyo wa Kiswahili katika huduma za afya kielektroniki kwa
kuzingatia madhumuni matatu: kubainisha aina za mifumo ya huduma za afya
kielektroniki zipatikanazo nchini Kenya; kutathmini matumizi ya Kiswahili katika
mifumo ya huduma za afya iliyokwisha bainishwa; na, kutathmini utayari wa watumiaji
wa mifumo ya huduma za afya kielektroniki kukitumia Kiswahili. Ili kushughulikia
vipengele vya kiteknolojia na kiisimu katika utafiti huu, nadharia mbili zilitumika.
Nazo ni: Nadharia ya Lugha za Mtandao na Nadharia ya Ukubalifu wa Teknolojia.
Nadharia ya Lugha za Mtandao ilisaidia kuchambua na kuelezea vipengele vya kiisimu jamii kuhusu matumizi ya Kiswahili katika huduma za afya kielektroniki. Aidha,
nadharia hiyo ilituwezesha kutathmini athari za teknolojia kwa Kiswahili, kwa upande
mmoja, na athari za Kiswahili kwa teknolojia, kwa upande mwingine. Nadharia ya
Ukubalifu wa Teknolojia ilitumika kutathmini urahisi wa matumizi pamoja na
manufaa-tarajiwa ya kukitumia Kiswahili katika dhana ya huduma za afya
kielektroniki. Utafiti elezi ulitumika na kwa kutumia mkabala wa mbinu-mseto
uliojumuisha njia za utafiti kitakwimu na zisizo za kitakwimu, data zilikusanywa kwa
njia tatu: dodoso, uchambuzi wa nyaraka na mahojiana. Data zilizotokana na dodoso
zilikusanywa kutika maeneo matatu nchini Kenya kwa kutumia dodoso iliyosambazwa
na kujazwa kimtandao. Madaktari wanne walihojiwa katika hospitali mbalimbali mjini
Eldoret ilhali data za uchanganuzi wa nyaraka zilitokana na programu 21 za huduma za
afya kielektroniki zipatikanzo nchini Kenya. Usimbaji kidhamia ulitumika
kuchanganua data za kitakwimu na takwimu elezi zilitumika kuchanganua data zisizo
za kitakwimu na matokeo yakawasilishwa kwa michoro, majedwali na vielelezo.
Ufasiri na mjadala kuhusu data vilionyesha kwamba programu za kiafya za rununu
hupatikana na kutumiwa nchini Kenya. Hata hivyo, kiwango cha upatikanaji wa
Kiswahili kwa jumla katika programu hizi ni 42.9% ilhali upatikanaji wa maandishi
kwa Kiswahili ni 9.5%. Uchunguzi huu pia ulidhihirisha kwamba ingawa wahudumu
wa afya na wagonjwa huenda wangependelea kutumia Kiswahili katika kushauriana,
kuna uhaba wa ufahamu kuhusu uwepo wa istilahi za kiteknolojia zinazorejelea
masuala ya afya kwa Kiswahili. Kwa sababu hiyo, Kiingerezakiliteuliwa na kutumiwa
katika miktadha ya mashauriano na utambuzi wa kimatibabu. Utafiti huu ulihitimishwa
kuwa, kwa sasa, Kiswahili si lugha ya msingi yanayotumika katika programu za kiafya
za rununu nchini Kenya. Utafiti unapendekeza kwamba programu zilizopo za programu
za kiafya za rununu zinafaa kutiwa msasa ili kujumuisha Kiswahili kama mojawapo ya
lugha za kuteuliwa mteja anapofungua programu hizi. Pia utafiti unatoa wito wa kupitia
tena na kutekeleza pendekezo la kufundisha Kiswahili kama somo la lazima kwa
taaluma zote za vyuo vikuu nchini Kenya mintarafu ya ripoti ya Tume ya Mackay ya
1981.