Abstract:
Utafiti huu ni uchanganuzi wa lugha ya amani na maridhiano katika muziki nchini Kenya
(2008-2012). Ulilenga kuchanganua matumizi ya kipekee ya lugha na jinsi maudhui ya
amani na maridhiano yanavyowasilishwa katika muziki tuliouteua. Utafiti huu
ulichanganua upekee katika uteuzi wa maneno, vishazi na sentensi kwa kuzingatia
uhusiano wa vipengele hivi kiwima na kimlalo. Unatanguliza kwa kueleza misingi ya
utafiti na uamilifu wa muziki kisiasa, kiuchumi na kijamii. Aidha, umeangazia matumizi
ya kipekee ya lugha katika uwasilishaji wa ujumbe wa amani na maridhiano jinsi
maudhui ya amani na maridhiano yameumbwa na kuwasilishwa ndani ya jumbe anuwai
kwenye muziki ulioteuliwa. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kubainisha muziki
uliotumiwa kuendeleza amani na maridhiano nchini Kenya kati ya mwaka wa 2008 na
2012, kupambanua matumizi ya kipekee ya lugha katika ubunaji wa wanamuziki kwa
kuzingatia maneno, vishazi na sentensi na kufafanua ujumbe katika muziki wa amani na
maridhiano katika muziki nchini Kenya (2008-2012). Nadharia ya majukumu ya lugha ya
Halliday pamoja na mawazo ya Fairclough kuhusu uchanganuzi makinifu wa diskosi
yalitoa msingi wa kinadharia kwa utafiti huu. Uamilifu anuwai wa muziki katika
kuwasilisha maudhui ya amani na maridhiano umeangaziwa kwa kuuhusisha na
majukumu ya lugha. Ufasiri wa uteuzi wa lugha umechanganuliwa kwa kuzingatia
mawazo kuhusu uchanganuzi makinifu wa diskosi kama mchakato wa kijamii. Data ya
utafiti huu iliteuliwa kimakusudi. Nyimbo ishirini zisizo za kidini zilizoimbwa nchini
Kenya baina ya mwaka wa 2008 na 2012 zilichunguzwa. Mbinu ya unukuzi wazi
ilitumiwa ili kuzalisha data iliyochanganuliwa. Nimetumia maelezo ya kinathari katika
kuichanganua data. Utafiti huu ulibainisha kwamba kuna uteuzi wa kipekee wa lugha
katika uwasilishaji wa ujumbe wa amani na maridhiano. Aidha, imebainika kuwa uteuzi
huu aghalabu unatawaliwa na muktadha ambamo muziki unatungwa na kuchezwa
pamoja na uamilifu unaolengwa kutimizwa na wasanii mbalimbali. Isitoshe, kupitia kwa
utafiti huu imebainika kwamba lugha huweza kutekeleza majukumu mbalimbali katika
jamii. Majukumu haya ni kama vile: kuhimiza amani na maridhiano, kuionya jamii dhidi
ya mienendo inayotishia amani na maridhiano pamoja na kutoa wasia wa jinsi ya
kuhakikisha kwamba jamii inapata amani ya kudumu miongoni mwa majukumu
mengine. Utafiti huu ni mchango katika kuelewa jinsi lugha inaweza kutumika kwa
namna chanya ili kuleta maendeleo katika jamii. Utafiti unapendekeza kutambuliwa na
kupanuliwa kwa uamilifu wa muziki katika kuzungumzia masuala muhimu yanayoikabili
jamii.