Abstract:
Japo bunilizi nyingi za watoto katika fasihi ya Kiswahili zinabainisha sifa za
mwingilianotanzu kiumbo, hakuna utafiti ambao umeangazia suala hili. Utafiti huu
unachunguza namna mwingilianotanzu unachimuza maudhui katika fasihi bunilizi za
watoto. Malengo ya utafiti huu ni mosi; kupambanua namna tanzu mahsusi zinajenga
bunilizi teule za watoto. Pili, kuchanganua namna tanzu mahususi zinachimuza
maudhui katika bunilizi teule za watoto na tatu ni kuhakiki uamilifu wa maudhui
kwenye tanzu husika kwa mtoto Mwafrika katika mazingira yake. Ili kutimiza
malengo haya, utafiti uliongozwa na maswali yafuatayo: Kwanza, ni tanzu zipi
zinazojenga fasihi bunilizi za watoto wa daraja la tatu? Pili, ni kwa namna gani
vipengele vya mwingilianotanzu vinachimuza maudhui katika fasihi bunilizi teule za
watoto? Mwisho, tanzu na maudhui yanayowasilishwa kwa bunilizi teule yana
uamilifu upi kwa mtoto Mwafrika? Utafiti huu umejikita katika vitabu teule vya
watoto; Mchezo wa Mtelezo na Hadithi Nyingine (Nandwa, 2016), Kade na Katana
(Syokau, 2018), Mchezo wa Kobole (Momanyi, 2019), Kito Apepeta (Nandwa, 2013),
Sitaki Iwe Siri (Matundura, 2008), Hidaya (Namlola, 2019), na Msiba wa Kujitakia
(Kea, 2013). Nadharia ya Mwingilianomatini yake Kristeva (1960) na Nadharia ya
Uoniafrika ya Asante (1980) ndizo kiunzi cha utafiti huu. Kristeva (1960) anadai
kuwa matini siku zote huingiliana na kutegemeana. Ni kwa msingi huu ndipo utafiti
huu unachunguza namna tanzu anuwai zinaingiliana na kuchimuza maudhui katika
bunilizi teule za watoto. Kwa upande mwingine, Uoniafrika unasisitiza kuwa maisha
ya Mwafrika lazima yatathminiwe kwa kuzingatia mwonoulimwengu wake. Nadharia
hii ilituongoza kuhakiki namna tanzu zinazoingiliana katika bunilizi teule
zinamwangazia mtoto Mwafrika katika mazingira yake. Ukusanyaji wa data ya
kimsingi ulitokana na bunilizi saba za watoto. Sampuli ya kimakusudi ilitumiwa
kuteua bunilizi hizo. Data ilichanganuliwa kiufafanuzi kulingana na maswali ya utafiti
na mihimili ya nadharia za utafiti. Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kuwa
mwingilianotanzu ni mojawapo ya mbinu ya kisanaa inayochimuza maudhui kama
vile umaskini, dini, uzalendo, utangamano na mengine katika bunilizi teule. Utafiti
huu ni kichocheo kwa wahakiki wa fasihi ya Kiswahili kuchunguza namna
mwingilianotanzu unachimuza maudhui katika tanzu nyinginezo za fasihi andishi na
simulizi. Aidha, utafiti huu unachangia pakubwa katika kubainisha vigezo vya utunzi
hasa wa fasihi ya watoto katika Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika.