Abstract:
Kiswahili ni lugha ya Kibantu inayozungumzwa Afrika Mashariki. Hutafitiwa na
hufundishwa katika nchi mbalimbali barani Afrika na nje. Itifaki ya Muungano wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, inatambua Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya
kikanda. Aidha, katiba ya nchi ya Uganda ya 1995 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2005, hati maalumu za serikali kama vile “The government white paper” ya 1992,
zinatoa matamko bayana kuhusu uendelezaji wa Kiswahili nchini Uganda. Licha ya
matamko ya kikatiba na mapendekezo kutoka hati mbalimbali za serikali, maendeleo
ya Kiswahili nchini Uganda, hayajaenda sambamba na ya nchi nyingine za Muungano
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hivyo, utafiti huu ulilenga kuchunguza
mchango wa sera ya lugha ya elimu katika uendelezaji wa Kiswahili nchini Uganda.
Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo: kujadili nafasi ya sera ya lugha katika
ukuzaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda, kufafanua changamoto
zinazokumba ukuzaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda na
kufafanua suluhu za changamoto zinazokumba ukuaji wa Kiswahili kupitia mfumo
wa elimu nchini Uganda. Data zisizo za kitakwimu zilikusanywa katika utafiti huu
huku usampulishaji wa kimaksudi ukitumika kwa watafitiwa kumi na watatu kutoka
taasisi za serikali na za binafsi jijini Kampala. Njia ya upekuzi wa nyaraka maktabani
na uchambuzi wa data za kiyaliyomo zilitumika. Aidha, mahojiano na maafisa kutoka
taasisi zilizohusika yalifanywa. Hali kadhalika, Nadharia ya Upangaji Lugha ya Einer
Haugen ilitumika katika utafiti huu. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa kuna
nyaraka nyingi za sera, maagizo na matamko ambayo yanakipa Kiswahili hadhi ya
kukuzwa na kuendelezwa kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda. Hata hivyo, hali
hii inakwamishwa na changamoto kama vile: ukosefu wa mikakati ya kutekeleza sera
za lugha kuhusu Kiswahili, ukosefu wa utashi thabiti wa kisiasa, mvutano na
mashindano kati ya lugha za kiasili na Kiswahili, mtazamo hasi kwa Kiswahili,
serikali kutoajiri walimu wa kutosha wa Kiswahili na uhaba wa vifaa vya kufundishia
shuleni. Suluhu za changamoto zinazokumba ukuzaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa
elimu zilizojadiliwa ni: serikali kuwekea mkazo utekelezaji wa sera kuhusu lugha ya
Kiswahili, kuunda baraza la Kiswahili la kitaifa, kuhamasisha watu kwa wingi kuhusu
manufaa ya Kiswahili, kuandaa warsha za kuboresha mbinu za ufundishaji kwa
walimu wa Kiswahili, kuandaa na kutoa vifaa vya kutosha vya kufundishia na
kujifunzia, kuthamini mtaala mpya wa sekondari unaozingatia umilisi na kuandaa vituo vya kujifunzia Kiswahili katika jamii. Matokeo ya utafiti huu ni muhimu kwa;
watunga sera na wapangaji lugha, wakuza mitalaa na wadau wengine katika sekta ya
elimu kuhakikisha utekelezaji wa mikakati mwafaka ya ukuzaji wa Kiswahili kupitia
elimu. Utafiti huu pia unachangia maarifa yaliyopo kuhusu sera na mipango ya lugha
pamoja na maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda katika mipaka ya elimu. Isitoshe,
matokeo ya utafiti huu yatakuwa msingi wa tafiti za baadaye kuhusu masuala ya sera
ya lugha pamoja na maendeleo ya Kiswahili kupitia mawanda mengine kama
utamaduni, bungeni, biashara na kwingineko.