Abstract:
Tamasha za drama ambazo hufanywa kila mwaka nchini Kenya ni mojawapo ya nyenzo
zilizowekwa na wizara ya Elimu nchini kutoa elimu kwa vijana. Tamasha hizi ambazo
zinajumuisha wanafuzi kutoka shule za malezi, msingi, sekondari, vyuo anuai na vyuo vikuu
hufanyika kila mwaka. Tamasha huanzia mashinani na kilele huwa kujumuika kwa timu ambazo
zimeshinda katika ngazi mbalimbali kwa mashindano ya kitaifa ambayo aghalabu hufanyika
mwezi wa Aprili. Mojawapo ya malengo ya tamasha hizi ni ustawishaji wa lugha za Wakenya
miongoni mwa wanaoshiriki. Tanzu mbalimbali kama michezo ya kuigiza, ngoma, mashairi,
sarakasi na masimulizi huwasilishwa. Washiriki huwa na uhuru wa kuwasilisha chochote
wanachokiwasilisha kwa lugha yoyote kuanzia Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za
Kenya. Hata hivyo, imebainika kuwa kazi nyingi ambazo hupata matuzo ni kazi katika lugha ya
Kingereza. Makala hii inalenga kuchunguza kiwango cha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika
tanzu zinazowasilishwa hasa katika ngazi ya kitaifa. Makala itachunguza tanzu zinazowasilishwa
kwa lugha ya Kiswahili huku ikilinganisha zinazowasilishwa kwa lugha ya nyingine ili
kubainisha ni kwa nini tanzu kwa lugha ya Kiswahili hazifikii kupata matuzo. Aidha, makala
itachunguza iwapo katika tamasha hizi, Kiswahili hupata nafasi ya kustawi au kudumaa.