Abstract:
Mhadhara huu unajadili lugha kama bidhaa yenye sifa za uamilifu changamano. Ni bidhaa ambayo ina umuhimu na thamani ya kisarafu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kwa hivyo inahitaji kupangiwa, kuendelezwa, kudumishwa na kuwekezewa. Miktadha mikuu mitatu inazingatiwa katika mjadala ili kujeleza, kufafanua, na kujenga tasnifu ya mhadhara huu. Ili kuweka usuli na kujenga msingi wa mjadala, diskosi inaendelezwa kuhusu dhana za kubidhaaisha na kuwekeza katika lugha ili kuiwezesha kutimiza majukumu ya kisarafu. Kiswahili kama lugha na bidhaa ya kiuchumi inajadiliwa hasa katika muktadha wa kubainisha sifa zake za kisarafu. Muktadha wa pili wa mhadhara unatalii asili na maendeleo ya Kiswahili katika akademia, taaluma ambayo inategemea lugha kama malighafi kimaarifa na kiutendaji. Hapa, mjadala unabainisha upeo na maarifa yaliyomo katika taaluma hii, kwa kuonyesha asili ya kuibuka, kubadilika na kuendelea kwake huku ikikabiliana na changamoto za masuala-ibuka ambazo zilizidi kuiimarisha kama bidhaa ambayo thamani yake ilizidi kukua na utoaji wa huduma kuimarika. Isitoshe, mjadala pia unatalii Kiswahili kama bidhaa katika soko la viwandani; kama nyenzo na chombo cha utoaji wa huduma kwa ajira na utimizaji wa mahitaji ya kiuchumi; na taathira zake ambazo zinaingia hatua kwa hatua katika mitaala ya kiakademia. Hatimaye mhadhara unajadili tafrisi kama namna mojawapo ya kubidhaaisha na kuendeleza uamilifu wa Kiswahili kama sarafu ya kijamii na kiuchumi. Katika hatua hii, tafsiri inazingatiwa kama uwanja maalum wa usomi na pia kama nyenzo ya kuendeleza michakato ya lugha. Mielekeo yenye kushinikiza utangamano wa kitaaluma wenye kushirikisha huduma za Kiswahili na taaluma nyingine; na sifa yake ya uamilifu wa kidarajia baina ya jamii lugha ili kusambaza habari na maarifa zinazingatiwa pia.