Abstract:
Mviga ni mchakato wa kiutamaduni unaohusisha matambiko yanayotekelezwa kupitia
kwa ibada maalum. Utafiti huu ulichunguza mviga wa maridhiano miongoni mwa
jamii ya Wanandi kama kipera cha utanzu wa maigizo katika fasihi simulizi. Utafiti
huu ulilenga kubainisha mchakato wa mviga huo kama kipera cha utanzu wa maigizo
katika fasihi simulizi, ukachunguza uamilifu wake katika jamii ya Wanandi na
kutathmini nafasi yake katika kusuluhisha migogoro katika karne ya ishirini na moja.
Malengo ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza mchakato wote wa mviga wa
maridhiano kama kipera cha fasihi simulizi katika jamii ya Wanandi, kubainisha
utendaji wake, na kutathmini nafasi yake katika katika karne ya 21 miongoni mwa
Wanandi. Utafiti huu uliendeshwa katika tarafa ya Kipkaren na Kabiyet katika kaunti
ya Nandi. Mbinu ya usampuli wa kimakusudi na elekezi ilitumika katika kuteua
wasailiwa. Uteuzi wa wasailiwa uliongozwa na sampuli elekezi na ya kimakusudi.
Data ilikusanywa kwa kutumia hojaji, utazamaji shiriki, na mahojiano kuhusu mviga
wa maridhiano ambayo yalirekodiwa kwa kutumia vinasa sauti na mengine
kunakiliwa kwa kutumia kalamu na karatasi. Data iliyokusanywa ilinukuliwa na
kutafsiriwa kutoka kwa lugha ya Kinandi hadi Kiswahili, ikasimbwa na
kuchanganuliwa kimaelezo kwa kuongozwa na nadharia ya uamilifu kama
ilivyopambanuliwa na Radcliff-Brown (1930) ambayo ilituwezesha kuchanganua
mchakato wa mviga wa maridhiano na nafasi ya mviga huu katika karne ya 21. Vile
vile, nadharia ya utendaji kwa mujibu wa Foley (1995) ilituongoza kubainisha
utendaji katika utekelezaji wa mviga wa maridhiano. Utafiti huu ulidhihirisha
kwamba katika utekelezaji wa mviga wa maridhiano kama kipera cha fasihi simulizi,
mchakato maalum wa kihatua hufuatwa. Aidha, katika utekelezaji wake kuna utendaji
unaohusisha matendo mbalimbali, uimbaji, na hata kuboboja maneno. Pia ilibainika
kwamba unatumika kuwapatanisha wanajamii, kutakasa, kutahadharisha, kutoa
mafunzo na kusisitiza ushirikiano. Vile vile, ilibainika kwamba, katika karne ya 21,
hatua za utekelezaji wa mviga huu zingali zinazingatiwa japo baadhi ya vyombo vya
utekelezaji wake vimebadilika. Tasnifu hii inapendekeza kuwa tafiti zaidi zifanywe
katika kipera hiki cha mviga wa maridhiano katika jamii nyingine k.v. jamii ya
Waluhya na Wajaluo. Vile vile, tafiti zifanywe kuhusu aina nyinginezo za miviga k.v.
mviga wa kutawaza kiongozi, harusi, mviga wa matanga/mazishi, mviga wa kumpa
mtoto jina n.k. Aidha, mwelekeo tulioutumia unaweza ukatumiwa kuchunguza tanzu
na vipera vingine vya fasihi simulizi k.v. ngomezi, visasili, masimulizi, vitendawili,
methali, nyimbo miongoni mwa nyinginezo.