Abstract:
Uongozi ni dhana muhimu sana katika jamii. Jamii zote ulimwenguni huwa na kiongozi
wa aina fulani ambaye hutwikwa majukumu ya kuhakikisha kuwa watu wote walio
chini yake wanapokea usawa kutokana na uongozi wake. Swala la uongozi
limeshughulikiwa katika kazi za fasihi kwa namna tofauti tofauti. Utafiti huu uliangazia
taswira ya uongozi inavyojitokeza katika fasihi ya kisasa kwa kuchunguza riwaya mpya
za miaka ya 2000. Uliangazia mwelekeo mpya ambao unakisiwa umechukuliwa na
baadhi ya waandishi wa riwaya mpya wanaoliona suala hili kwa mtazamo wa ndani nje.
Madhumuni yafuatayo yalizingatiwa: Kufafanua taswira ya uongozi kama
inavyosawiriwa na riwaya mbili mpya kwa kuangazia matatizo ya uongozi katika asasi
za siasa na dini; Kutathmini mchango wa wananchi katika uongozi kwa mujibu wa
riwaya zilizoteuliwa; na kuchunguza mtazamo wa ndani nje na mapendekezo
yanayotolewa na riwaya kukabiliana na changamoto za uongozi. Riwaya za Msimu wa
Vipepeo Wamitila (2007) na Paradiso Habwe (2010) ziliteuliwa. Data ilikusanywa
kupitia usomaji makini wa riwaya zilizoteuliwa kwa kuzingatia mawazo ya waandishi
yawe hasi au chanya kuhusu uongozi kwa kutumia uchambuzi wa yaliyomo. Utafiti huu
uliongozwa na nadharia ya uhistoria mpya. Data ilipangwa na kuchanganuliwa
kimaelezo hivi kwamba mada zinazohusiana ziliwekwa na kuhusishwa kwa kijumla
kama maoni ya waandishi kuhusu uongozi katika kipindi hiki maalum cha kihistoria.
Utafiti huu umegundua kuwa uongozi bado ni changamoto katika asasi tofauti za
kijamii na hasa katika siasa, serikali na dini ambazo zilishughulikiwa na riwaya
zilizoteuliwa. Uongozi una athari za moja kwa moja katika maendeleo ya jamii na
kwamba watawaliwa wanachangia tatizo hili. Waandishi wameonyesha kuwa ni lazima
viongozi wayaangazie matatizo ya jamii kwa kushauriana na jamii badala ya
kujiangazia wao binafsi. Pia, wananchi lazima wahakikishe kuwa viongozi
wanawajibika kwa kujihusisha na masuala ya uongozi nchini. Katika dini, waandishi
wanataka asasi hiyo iweze kujirekebisha kwa kuangazia maadili ya kidini ili jamii
iwachukulie kwa dhati.