dc.description.abstract |
Ukiukaji wa kanuni za kitahajia na kisarufi katika lugha husababisha makosa. Makosa
yanayofanywa na wanafunzi wa shule husababisha matokeo duni katika mitihani.
Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) hutathmini watahiniwa katika kiwango cha
Elimu ya Msingi na Kiswahili ni kati ya masomo ya lazima yanayotahiniwa katika
kiwango hiki. Katika siku za hivi karibuni, hasa kati ya 2016 na 2018, utendaji wa
wanafunzi katika somo la Kiswahili umekuwa ukizorota na makosa ya kitahajia na
kisarufi ni sababu mojawapo ya kudorora huku. Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa
kuhakiki makosa katika maandishi ya wanafunzi wa shule za upili katika kaunti
ndogo ya Likuyani, kaunti ya Kakamega na katika baadhi ya vitabu vya kiada vya
Kiswahili. Malengo mahsusi yalikuwa ni kutambua na kuchanganua makosa ya
kitahajia na kisarufi katika maandishi ya wanafunzi na vitabu vya kiada. Tuliongozwa
na nadharia tete kwamba makosa katika maandishi na vitabu vya kiada hujidhihirisha
kwa namna mbalimbali na kwamba makosa kwenye maandishi ya kiada huigwa na
wanafunzi. Tuliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa iliyofasiliwa na S. P.
Corder. Utafiti huu ulifanywa nyanjani na maktabani ambapo tulizuru Shule tisa za
Upili katika eneo la utafiti na kusoma vitabu vitatu vya kiada maktabani. Mazoezi
matatu ya kuandika yenye Viasho, Jozi za Mlinganuo Finyu na Insha, yalitumiwa ili
kupata data ya uchanganuzi. Kwa kufanya utafiti maktabani, tulipata data ya makosa
katika vitabu vya kiada. Data ilichanganuliwa kwa kuzingatia utukiaji wake chini ya
vipengele vya udondoshaji, uchopekaji na ubadilishaji wa herufi na maneno. Aidha,
tulizingatia utenganishaji na uunganishaji wa maneno katika kitengo cha makosa ya
kitahajia. Upatanisho wa kisarufi, minyambuliko na uambishaji ni vipengele vingine
tulivyozingatia katika kuchanganua data kuhusu makosa ya kisarufi. Matokeo ya
utafiti yalidhihirisha kwamba wanafunzi walifanya makosa yanayofanana na makosa
yanayopatikana kwenye vitabu vya kiada. Makosa mengine yalitokana na athari za
lugha ya kwanza ya wanafunzi. Tunapendekeza kwamba kadiri tunavyojitahidi
kukabiliana na athari za lugha ya kwanza kama sababu kuu ya makosa katika
Kiswahili, ni sharti kuwe na umakinifu katika uandishi wa vitabu vya kiada kwani
makosa yanapokuwamo, huwa na athari hasi kwa wanafunzi. Kushughulikiwa kwa
visababishi hivi kutapunguza makosa ya wanafunzi na kuimarisha utendaji wa
wanafunzi katika mitihani ya Kiswahili. |
en_US |