Abstract:
Utafiti huu unahusu usawiri wa mwanamke katika kazi teule za fasihi na jinsi
maandiko ya kidini yanavyomwangalia mwanamke katika jamii. Kazi hizi teule za
fasihi ni Utendi wa Mwanakupona (1858), Utendi wa Ayubu (1723) na maandiko ya
kidini ya ‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’ katika Biblia Takatifu, Agano la
kale (1921). Katika utafiti huu, tumelinganisha mwanamke anavyosawiriwa katika
kazi hizi mbili za fasihi na maandiko matakatifu yanavyotarajia tabia na uhusiano wa
mwanamke na mwanamume katika ndoa. Waandishi wengi kwa kuathiriwa na
Ufeministi na usawa wa kijinsia, wamemsawiri mwanamke aliyedhalilishwa na
kunyanyaswa katika ndoa. Katika utafiti wetu, tumechunguza miongozo inayotolewa
katika tendi hizi na kulinganisha na mwongozo wa kidini unaotolewa kupitia ‘Kitabu
cha Methali na Wimbo Ulio Bora’. Mwanamke anaposimamia nafasi yake katika
ndoa sio ukandamizaji bali utekelezaji wa majukumu yake katika ndoa. Kwa hivyo,
tumechunguza iwapo yapo manufaa katika Utendi wa Mwanakupona, Utendi wa
Ayubu, ‘‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’’ katika kukuza na kuujenga
uhusiano madhubuti katika ndoa. Ili kuendeleza utafiti huu, tuliteua sampuli ya
kimakusudi iliyoafikiana na malengo yaliyoongoza utafiti huu. Malengo kwenye
tasnifu hii ni kuchanganua taswira ya mwanamke kutoka kazi hizi teule za fasihi na
matini za dini, kutathmini uhusiano wa mwanamke na mwanamume katika Utendi wa
Mwanakupona, Utendi wa Ayubu, ‘‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’’, na
kubainisha dini kama kigezo muhimu katika uthabiti wa ndoa. Maktabani, utafiti huu
ulipata data katika kazi teule za Utendi wa Mwanakupona, Utendi wa Ayubu, ‘Kitabu
cha Methali na Wimbo Ulio Bora’. Data hii ilichanganuliwa kwa kutumia takwimu
fafanuzi. Fasiri na mitazamo mbalimbali imetolewa na waandishi wengi kuhusiana na
kazi zetu tulizozichagua na kuhitimisha kuwa mwanamke amekandamizwa na
kudhalilishwa. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Ufeministi na nadharia ya
Udenguzi. Nadharia ya Ufeministi huangazia jinsi mwanamke amenyanyaswa katika
jamii na mbinu zinazoweza kumkomboa. Nadharia ya Udenguzi inadai kuwa kila
tamko lina sura mbili, sura iliyopo na sura ya kupangua wakati ule ule mmoja.
Mahitimisho ya utafiti huu ni kuwa mwanamke ana nafasi yake maalum katika jamii
kama mpenda amani, kielelezo bora kwa watoto na familia kwa jumla. Utafiti huu
vile vile ulibainisha mihimili muhimu inayojenga familia kama vile kusameheana,
kufurahishana n.k na kwamba mwanamke na mwanamume wanastahili kuishi pamoja
licha ya changamoto na matatizo ya maisha. Ilibainika wazi kuwa Mungu ndiye
mwanzilishi wa familia na angependa waliooana waishi kwa amani, na kwa hivyo
dini ni kigezo muhimu katika ndoa. Kwa jumla, utafiti huu una mchango mkubwa
katika taaluma ya Kiswahili na jamii. Katika utafiti huu tumeonyesha kwamba wosia
katika Utendi wa Mwanakupona, taswira ya mwanamke katika Utendi wa Ayubu na
matini ya kidini si ukandamizaji wa mwanamke bali ni njia ya kuujenga uhusiano
mwema katika ndoa. Wafuasi wa dini hizi mbili wakiyazingatia maelekezo kutoka
kwa kazi hizi, basi itakuwa ni mchango mkubwa katika kuimarisha ndoa. Aidha,
umechangia katika fasihi ya Kiswahili, Waswahili kama jamii na jamii nyingine
duniani, wasomaji na wahakiki wa fasihi ya karne hii, kuziangalia kazi hizi upya, na
kwamba zina wosia bora zikijikita katika misingi ya kidini katika ndoa za leo.