Abstract:
Utafiti huu ulilenga kushughulikia umuhimu wa upole katika mazungumzo kwa
kuchanganua mikakati ya upole inayotumika katika vipindi vya Sobetab Kapchi
(Maisha ya Jamii) kwenye idhaa ya KASS FM. Ili kutekeleza jukumu hilo, utafiti
uliongozwa na madhumuni yafuatayo: kuchanganua mikakati ya upole inayotumika
kuwasilisha vipindi vya Sobetap Kapchi (SK) katika idhaa ya KASS FM, kuhakiki
athari za uzingatiaji na ukiukaji wa kanuni za upole kwenye vipindi vya SK,
kutathmini hali zinazoathiri uteuzi wa mikakati ya upole katika vipindi husika vya SK
na kupambanua na kujadili changamoto zinazosawiriwa na wahusika wa
mazungumzo ya SK wakati wa utekelezaji wa kanuni za upole. Aidha, utafiti
uliongozwa na maswali manne. Kwanza, je, ni mikakati gani ya upole inatumika
kuendeleza mazungumzo ya SK kwenye idhaa ya KASS FM? Pili, uzingatiaji au
ukiukaji wa mikakati ya upole una athari gani kwa mazungumzo ya vipindi vya SK?
Tatu, Ni hali zipi zinaathiri uteuzi wa mikakati ya upole katika mazungumzo ya
vipindi vya SK kwenye idhaa ya KASS FM? Mwisho, wahusika wa mazungumzo ya
SK wanasawiri changamoto zipi wakati wa kutekeleza mikakati ya upole? Utafiti
uliongozwa na Nadharia ya Upole, hasa mhimili wa ‘kuokoa uso’, kama
ilivyopendekezwa na Brown na Levinson. Kulingana na waasisi wa nadharia hii, uso
ni thamani ya kijamii ambayo mtu hujipa kulingana na atakavyo kuchukuliwa na
wengine. Unarejelea kile ambacho mtu anatamani katika mawasiliano yoyote.
Nadharia ya Upole inaeleza kuwa mtu ana aina mbili za uso; uso chanya na uso hasi.
Aidha, nadharia hii inasisitiza kuwa mawasiliano yoyote hufanikiwa iwapo washiriki
wa mazungumzo wanazingatia kanuni za upole kwa makusudi ya kuokoa nyuso zao
na za wenzao. Isitoshe, kila mshiriki wa mazungumzo anatakiwa kuhisi kukubalika na
kupewa uhuru wa kutoingiliwa. Sampuli ya utafiti iliteuliwa kimakusudi kuambatana
na nadharia ya utafiti, malengo na maswali ya utafiti pamoja na upeo wa utafiti kwa
kuangazia masuala mahsusi ya kipindi hiki kulingana na utamaduni wa jamii ya
Kikalenjin. ‘Pasta’ Edward Rotich na mwelekezi wa vipindi Winny Jepkorir
(‘Koriryo’), ni wahusika wakuu na pamoja nao ni mashabiki waliochangia katika
vipindi husika. Vipindi vya SK vilisikilizwa kwa makini kabla ya kunaswa. Kinasa
sauti kilitumika kukusanya data kwa kurekodi vipindi vinane vya SK. Mwisho, hoja
zinazohusiana na upole zilinakiliwa na kuwekwa kwenye makundi manne ya mikakati
ya upole ili kuchanganuliwa. Makundi hayo ni ya mkakati wa kuwa kwenye rekodi,
mkakati wa upole chanya, mkakati wa upole hasi na mkakati wa kuwa nje ya rekodi.
Uchanganuzi wa data ulifanywa kimaelezo kwa kutumia mazungumzo ya washiriki
kama mifano halisi. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa wahusika wa mazungumzo
ya SK hutumia mikakati anuwai ya upole kuwasiliana ili kudumisha mahusiano kati
yao. Pia, wahusika hao hukumbana na changamoto nyingi wanapotekeleza mikakati
ya upole wakati wa mazungumzo. Kutokana na matokeo hayo, utafiti huu ni matini
muhimu katika uwanja wa mawasiliano kwenye vyombo vya habari hasa vya
redio.Utafiti huu ni mchango mkubwa kwa taaluma ya isimu, hasa kwa wale walimu
na wanafunzi wa uamali na isimu-jamii, wanaotafitia suala la upole katika
mazungumzo kwenye vyombo vya habari katika lugha yoyote ya Kiafrika, hasa lahaja
za Kikalenjin. Pendekezo la jumla ni kuwa watafiti wajitokeze kushughulikia masuala
ya upole katika nyanja za fasihi na tafsiri.