Abstract:
Utafiti huu ulichunguza uleksikalishaji, ukriolishaji na mikakati ya kiwingi-lugha
ambayo hutumika katika ubadilishaji msimbo baina ya Sheng’ na Kiswahili.
Madhumuni ya utafiti yalikuwa kuhakiki mbinu za uleksikalishaji zinazotumiwa katika
Sheng’ kwa kuzingatia vigezo vya Pegitosca, kufafanua sifa zinazopinga upijini na
ukriolishaji wa Sheng’, kupambanua mikakati ya kiwingi-lugha inayojitokeza katika
diskosi zenye Sheng’ na kuchanganua tungo zenye Sheng’ kwa kuzingatia nadharia ya
4M. Utafiti wenyewe ulichunguza mbinu za uleksikalishaji na mikakati ya kiwingi-
lugha inayotumiwa katika diskosi zenye Sheng’ ili kudhihirisha iwapo msimbo wa
Sheng’ ni msimu, lahaja ya Kiswahili, lugha, sajili, Pijini au Krioli. Nadharia mbili
zilitumiwa katika utafiti huu: Kwanza, nadharia ya Pegitosca ya Kiingi ilitumiwa katika
uhakiki wa mbinu za uleksikalishaji zinazotumiwa katika Sheng’ na pili, nadharia ya
4M ya Myers-Scotton ilitumiwa ili kupambanua mikakati ya kiwingi-lugha na
kuchanganua tungo zenye Sheng’. Data ya utafiti huu ilikusanywa kutoka kwa Shule
tatu za upili zilizoteuliwa kimakusudi. Familia mbili za mitaani na makundi mawili ya
vijana wanaoishi mitaani kutoka mitaa miwili katika kaunti ya Kisumu walihojiwa. Ili
kuwafikia watafitiwa mahususi mitaani mbinu ya usampulishaji wa bonge-luji
ilitumiwa. Kiranja mmoja katika kila shule iliyoteuliwa alitumiwa kupata sampuli ya
wanafunzi 120 ambao walipewa karatasi na kuombwa waandike barua kwa marafiki
zao wakitumia lugha waipendayo. Vilevile diskosi baina ya wanafunzi hawa
zilirekodiwa. Katika sampuli ya familia za mitaani, mtafiti aliwahoji na akarekodi
diskosi za vijana na wazazi waliokuwa wakiishi katika mitaa miwili iliyoteuliwa.
Matokeo ya utafiti huu yamethibitisha kwamba Sheng’ ni msimu na si lahaja, Pijini,
Krioli wala lugha. Mbinu za kipekee za uleksikalishaji zinazotumiwa katika Sheng’,
ambazo hazikuwa zimebainishwa katika tafiti za awali kama ufinyaji wa maana na
uhamishaji wa maana ziligunduliwa katika uchunguzi huu. Matokeo hayo
yameonyesha kwamba mofimu nyingi amilifu zinazotumiwa katika mtagusano baina
ya msimbo wa Sheng’ na Kiswahili huwa za Kiswahili. Kuhusiana na mofimu nne (4M)
zinazoshiriki katika ujenzi wa miundo ya UM yenye Sheng’, iligunduliwa kwamba
Sheng’ hutumia mofimu amilifu za Kiswahili kwa vile haina mofimu zake amilifu. Hata
hivyo, Sheng’ ina mofimu chache amilifu ndiposa tasnifu hii ikahitimisha kwamba
msimbo wa Sheng’ ungeimarika kiasi cha kuwa na mofimu amilifu nyingi, huenda
ingeweza kutumiwa mara nyingi pia kama lugha solo. Tasnifu hii inapendekeza haja ya
kustawisha nadharia ya 4M ili iweze kufafanua pia miundo ya lugha mojamoja, na
nadharia ya Pegitosca ili itofautishe nguzo za kuchambua msamiati na istilahi.