Abstract:
Ushairi wa Kiswahili una historia ndefu kutokana na dhima yake katika jamii. Ukweli
ni kuwa historia hiyo inatokana na watunzi ambao wamechangia maendeleo ya utanzu
huu wa kifasihi. Wapo washairi wengi wa Kiswahili waliotunga mashairi katika
nyakati tofauti lakini mchango wa kazi zao haujajulikana kikamilifu katika taaluma ya
fasihi ya Kiswahili. Mmojawapo wa washairi waliosahaulika ni Mathias Mnyampala.
Azma kuu ya utafiti huu ni kuchunguza na kuchambua ushairi wa Mathias
Mnyampala kimwingilianomatini. Utafiti huu umelenga kuchunguza upekee wa tungo
za kishairi za Mathias Mnyampala na kuzihakiki mbinu za kifani zilizotumika kuibua
maudhui kwa kuzingatia muktadha wa utunzi wake kimwingilianomatini. Malengo ya
utafiti huu ni mosi, kupambanua muktadha wa utunzi uliomsukuma mwandishi
kutunga kazi teule za ushairi wa Kiswahili. Pili, kuhakiki mbinu za kifani
zinavyotumika kuibua maudhui katika kazi teule za ushairi za Mathias Mnyampala.
Tatu, kutathmini mchango wa kazi za ushairi za Mathias Mnyampala katika
maendeleo ya ushairi wa Kiswahili. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya
Mwingilianomatini. Mwingilianomatini ni nadharia iliyoasisiwa na Julia Kristeva
miaka ya 1960. Nadharia hii inasisitiza kuwa hakuna matini asilia, bali uhai wa matini
moja hutegemea matini nyingine tangulizi. Hivyo basi, matini za fasihi hutegemeana
katika kukamilisha maana. Ni kwa msingi huu ndipo uhakiki wa mashairi ya Mathias
Mnyampala yamechanganuliwa kimwingilianomatini. Kwa kutumia nadharia hii
tumebaini kuwa kazi za Mnyampala zinaingiliana, zinakamilishana na kutegemeana
na matini nyingine tangulizi. Utafiti huu ni wa maktabani na nyanjani. Kutoka
maktabani, data ilikusanywa kutoka kazi teule zilizochapishwa ambazo ni: Diwani ya
Mnyampala (1965), Mashairi ya Hekima na Malumbano ya Ushairi (1965) na
Ngonjera za UKUTA Na. 1 (1970). Kutokana na mahojiano ya watafitiwa nyanjani
tulipata data kuhusu maisha na historia ya Mnyampala pamoja na miswada yake
isiyochapishwa ifuatayo: Hazina ya Washairi, Mahadhi ya Kiswahili na Mashairi ya
Vidato. Usampulishaji makusudi ulitumika kuteua kazi tatu zisizochapishwa na
usampulishaji nasibu ulitumika kuchagua kazi tatu zilizochapishwa. Data
zilichambuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo ya kina yaliyohusisha udondozi
na ufafanuzi wa mistari, beti na vifungu vya maneno. Uchambuzi huo unadhihirisha
mwingilianomatini wa fasihi simulizi na tamaduni za kisasa katika mashairi ya
Mathias Mnyampala. Utafiti huu unadhihirisha kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati
ya muktadha wa utunzi, mbinu za kifani na uibuaji wa maudhui ya kazi teule za
Mathias Mnyampala. Matokeo ya utafiti ni kwamba, Mathias Mnyampala amechangia
pakubwa katika maendeleo ya ushairi wa Kiswahili. Mojawapo ya mchango wake ni
kuongozwa na Nadharia ya Kimapokeo katika utunzi wa mashairi yake.
Wanamapokeo wanasisitiza upekee wa shairi la Kiswahili kimuundo hasa urari wa
vina na mizani. Kwa kutumia nadharia hii, Mathias Mnyampala aliibua mbinu mpya
za utunzi mfano mbinu ya mtiririko na msisitizo. Kupitia utafiti huu tumevumbua
miswada, barua na nyaraka mbalimbali za kifasihi zilizotungwa na Mathias
Mnyampala zenye mchango mkubwa katika ushairi, fasihi na Kiswahili kwa ujumla.
Miswada hiyo ni malighafi ya tafiti za kifasihi na machapisho ya kitaaluma.