Abstract:
Taaluma ya tafsiri inajumuisha si tu kubadilisha maneno kutoka lugha moja hadi
nyingine, bali pia kuhamisha na kutafsiri maadili, desturi na mitazamo mbalimbali ya
kitamaduni. Utafiti huu ulikusudia kueleza na kuchanganua jinsi uhifadhi wa
utamaduni umeendelezwa kupitia tafsiri ya riwaya za Kaburi Bila Msalaba (Kareithi)
na Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali (Kitereza). Utafiti
uliongozwa na madhumuni matatu: kubaini vipengele vya kitamaduni katika matini
teule, kutoa maelezo yanayothibitisha kwamba riwaya hizi mbili ni hazina ya hifadhi
ya utamaduni wa maisha ya jamii mahususi za Kiafrika; kujadili na kuitathimini
michakato na mikakati iliyotumiwa kutafsiri kazi chanzi kama mikakati ya uhifadhi
wa utamaduni katika riwaya hizi mbili; kuonyesha jinsi udumishwaji wa baadhi ya
vipengele vya lugha chanzi (Kiswahili na Kikerewe) unavyoweza kufasiriwa kama
ithibati ya uhifadhi wa utamaduni katika tungo asilia na katika tafsiri. Utafiti huu
uliongozwa na nadharia mbili: nadharia ya anthropolojia na nadharia ya Skopos.
Nadharia ya anthropolojia ilizingatia tapo la isimu anthropolojia ambalo linachunguza
tabia na mienendo ya watu na jinsi wanavyotumia lugha kwa lengo la kuonyesha
ukweli na uhalisia wa mambo katika jamii. Nadharia ya Skopos huchukulia shughuli
ya kutafsiri kama kitendo kilicho na malengo. Yaani, kabla mtafsiri hajaanza kazi
yake ni sharti aelewe lengo la tafsiri yake. Utafiti ulikuwa wa maktabani. Mtafiti
alijikita katika riwaya za Kareithi na Kitereza na tafsiri zao katika lugha ya
Kiingereza. Matini teule zilisomwa na data msingi kurekodiwa. Data ilipangwa na
ilichanganuliwa kulingana na malengo ya utafiti na matokeo yaliwasilishwa kwa njia
ya maelezo. Kuhusu lengo la kwanza, utafiti uligundua kwamba fasihi haiumbwi
katika ombwe tupu bali hufungamanishwa na maisha ya binadamu na mazingira yake.
Dhana za kitamaduni zinapotafsiriwa huwa ni njia moja ya kuhifadhi utamaduni kwa
hadhira lengwa. Mintarafu ya lengo la pili, utafiti ulibaini kwamba mikakati maalum
ilitumiwa ili kuhawilisha vipengele vya kitamaduni kutoka matini chanzi hadi hadhira
lengwa jinsi nadharia ya Skopos inavyoweka. Vipengele vingi vya kitamaduni katika
matini asilia viliweza kudumishwa kupitia mikakati mbalimbali ya tafsiri. Kulingana
na lengo la tatu, utafiti ulionyesha kwamba mbinu nyingi za ujielezaji hufungamana
na utamaduni na miktadha ya kila siku ya jamii husika. Mbinu hizi zinapohawilishwa
mikakati maalum hushirikishwa na hii huwa ni njia moja ya kuhifadhi utamaduni
kupitia mchakato wa tafsiri. Utafiti ulihitimisha kwamba uhifadhi wa utamaduni
unawezeshwa kupitia mchakato wa tafsiri. Utafiti huu unapendekeza kuwe na tafiti
zingine zinazozingatia maandishi ambayo hayakushughulikiwa katika utafiti huu
kama vile tamthilia na hadithi fupi. Aidha, utafiti unaweza kufanywa kwa kutumia
nadharia tofauti kando na nadharia ya anthropolojia na nadharia ya Skopos.