Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/8585
Title: Utendaji Katika Nyimbo za Ngoma ya Wasambaa: Mifano Kutoka Mdumange Nchini Tanzania
Authors: Ramadhani, Thomas Kadallah
Keywords: Teknolojia
Issue Date: 2018
Publisher: Moi University
Abstract: Licha ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na habari bado turathi za kifasihi simulizi zikiwemo nyimbo zingali zinaheshimiwa na jamii nyingi za Kiafrika kwa kuwa ni tunu inayotumika kuhifadhi historia, kuendeleza amali za jamii na pia ni chemchemi ya burudani. Kutokana na umuhimu wa nyimbo katika jamii, utafiti huu umechunguza utendaji wa nyimbo za mdumange kutoka jamii ya Wasambaa wa Lushoto, Tanga – Tanzania kwa minajili ya kutathmini nafasi ya utendaji wa nyimbo za mdumange katika mwonoulimwengu wa Wasambaa. Madhumuni mahsusi ya utafiti huu yalikuwa: (i) Kupambanua jinsi miktadha ya kijamii inavyochochea utendaji wa nyimbo za mdumange; (ii) Kuchanganua usawiri wa maisha ya Wasambaa kupitia mitindo ya lugha inayotumika katika nyimbo za mdumange na; (iii) Kujadili nafasi ya mitindo ya viziada lugha kwa wasanii wa nyimbo za mdumange na jamii ya Wasambaa kwa ujumla. Data zilikusanywa nyanjani kwa kutumia mikakati ya uchunguzi shiriki, usaili na mijadala ya vikundi. Vifaa vilivyotumika vilikuwa kamera, kinasa sauti na redio kaseti. Uchambuzi wa data uliongozwa na Nadharia za Utendaji wa Maigizo pamoja na Semiotiki ya Kijamii. Kulingana na Nadharia ya Utendaji wa Maigizo, utendaji ni tukio la aina yoyote ile linalowajumuisha hadhira pamoja na fanani wake kwa minajili ya kuigiza au kuonyesha tabia za wanadamu. Nadharia hii ilichaguliwa kwa kuwa katika jamii nyingi za Kiafrika utendaji ni mojawapo ya kanuni za maisha ya kila siku. Kutokana na mihimili ya Nadharia hii, utendaji unachukuliwa kuwa ndicho kiungo cha fasihi simulizi chenye uwezo wa kudhihirisha ujumi na diskosi za wanajamii. Kwa upande mwingine, Nadharia ya Semiotiki ya Kijamii ilitumika kwa minajili ya kupambanua misimbo au ishara zinazohusika wakati wa utendaji. Wafuasi wa Nadharia hii wanaeleza kuwa Semiotiki huchunguza maana katika ishara pamoja na kuonyesha uhusiano kati ya ishara husika na mifumo mbalimbali ya jamii. Kimsingi, kupitia utafiti huu imegundulika kuwa nyimbo za mdumange ni sanaa thabiti ya Wasambaa iliyosheheni vipashio mbalimbali vya ujumi, hususan lugha na viziada lugha. Kadhalika, kupitia utafiti huu imedhihirishwa kuwa utendaji wa fanani na hadhira unaimarishwa na mitindo ya lugha na viziada lugha. Kwa kutumia mitindo hiyo, fanani na hadhira wanajadili itikadi mbalimbali za maisha ya Wasambaa kijamii, kisiasa, na kiuchumi. Kwa ujumla, utafiti huu umegundua kuwa utendaji wa nyimbo za mdumange umekuwa ukichochewa na miktadha anuai ya Wasambaa kama vile turathi simulizi, mwingiliano na jamii nyingine pamoja na mfumo wa maisha ya Wasambaa unaodhihirika kwenye sherehe za harusi, dini na siasa. Imegundulika pia kuwa utendaji wa nyimbo za mdumange una nafasi kubwa katika jamii ya sasa ya Wasambaa. Nyimbo hizo hutumika kwa minajili ya kuburudisha, kuelimisha, kuhifadhi turathi na kufasiri mwonoulimwengu wa Wasambaa. Pamoja na matokeo haya, utafiti huu umependekeza kuwa ipo haja ya kuchunguza utendaji wa nyimbo nyingine za jamii, hususan nyimbo za maombolezo
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/8585
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
There are no files associated with this item.


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.