Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/7164
Title: Utamaduni, itikadi na utambulisho katika riwaya ya caitaani mutharaba-ini na tafsiri zake shetani msalabani na devil on the cross
Authors: Magugu, Vincent Njeru
Keywords: Utamaduni
Itikadi
Issue Date: 2022
Abstract: Katika kusoma riwaya ya Caitaani Mutharaba-ini iliyoandikwa na Ngũgĩ wa Thiong’o na tafsiri yake kwa Kiswahili, Shetani Msalabani na kwa Kiingereza, Devil on the Cross, inabainika kwamba kuna tofauti zinazojitokeza katika jinsi ujumbe umesimbwa na kuwasilishwa. Kando na kwamba tafsiri iliyotekelezwa imekiuka ubia wa kimapokeo katika utekelezaji na uhawilishaji wa maana, matini za Kiswahili na za Kiingereza zilizoangaziwa ni mazao ya tafsiri binafsi. Kwa jinsi hii, utafiti huu kwanza ulichanganua udhihirikaji wa utamaduni, itikadi na utambulisho katika riwaya ya Caitaani Mutharaba-ini. Utafiti aidha uliangazia jinsi dhana hizi zilishughulikiwa katika tafsiri za Shetani Msalabani na Devil on the Cross. Uchanganuzi uliangazia lugha hasa uteuzi wa kiisimu, vipengele vya fasihi simulizi na matumizi ya dhana zinazofungamana na utamaduni chanzi. Utafiti huu vilevile ulichunguza namna itikadi ilidhihirika kupitia kwa lugha katika riwaya hii na jinsi dhana hii ilihawilishwa katika tafsiri za Kiswahili na Kiingereza. Dhana ya utambulisho ilishughulikiwa kwa kuchunguza jinsi ilivyobainishwa katika Caitaani Mutharaba-ini na ilivyotafsiriwa kwa Kiswahili na Kiingereza. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili: nadharia ya Baadaukoloni katika tafsiri na nadharia ya Uchanganuzi wa Diskosi. Data ya utafiti ilikusanywa kwa kutumia usampulishaji wa kimakusudi ambapo usomaji hakikifu ulitekelezwa kwa matini husika kuambatana na azma na upeo wa utafiti huu. Data ilipangwa kwa utaratibu wa vigeu vilivyokuwa vikijadiliwa na uchanganuzi ukafanywa kwa njia ya maelezo. Uchanganuzi ulidhihirisha matumizi ya vipera vya fasihi simulizi pamoja na dhana zinazofungamana na utamaduni chanzi katika kuumba matini chanzi. Hali hii ilihusishwa na uteuzi wa kimakusudi ambao unabainika katika fasihi ya baadaukoloni. Katika kuchunguza tafsiri, ilibainika kuwa mtafsiri alichanganya baina ya mbinu ya uibuaji ugeni na ile ya ubinafsishaji katika kuhawilisha dhana hizi za kitamaduni. Aidha, uteuzi wa kiisimu aliofanya mtafsiri katika tafsiri ya Kiswahili na ile ya Kiingereza pakubwa ulibainishwa kuwa ulikuwa wa kimakusudi na uliongozwa na msukumo wa kiitikadi. Utambulisho ulibainishwa kuwa dhana ya kimsingi katika fasihi ya baadaukoloni na tafsiri yake ambapo mtafsiri anatumia lugha kwa njia ya kimakusudi kuumba utambulisho maalum na kuuhawilisha kadri ya dhima ya tafsiri yake. Kutokana na utafiti huu, ilidhihirishwa kwamba, tafsiri aghalabu ni mchakato changamano wa mawasiliano. Vilevile, tafsiri ni jukwaa ambapo mahusiano ya kiuwezo baina ya lugha na tamaduni tofauti hudhihirika. Hitimisho la utafiti ni kwamba lugha katika tafsiri za baadaukoloni hutumiwa makusudi kwa lengo la kukinza ubabe wa lugha na tamaduni za kibepari huku ikikweza tamaduni na lugha za waliowahi kutawaliwa. Utafiti huu umependekeza haja ya kitaaluma ya kutambua nafasi ya mtafsiri na athari yake katika mchakato wa tafsiri. Aidha, pana haja ya kutalii dhana ya itikadi kama kipengele cha kimsingi katika utekelezaji na katika taaluma ya tafsiri. Isitoshe, utafiti unapendekeza kwamba ni muhimu kuimarisha mwelekeo wa nadharia ya baadaukoloni katika tafsiri kwa kujumuisha ndani mwake vipengele vya uchanganuzi wa diskosi ili kuwezesha uchanganuzi wa kina. Mwisho, pana haja ya kuzidi kupanua upeo wa utafiti katika taaluma ya tafsiri kwa Kiswahili kwa kuchunguza vipengele zaidi vya ulinganifu katika tafsiri na ubora wa tafsiri.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/7164
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
MAGUGU Vincent 2022.pdf2.31 MBAdobe PDFView/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.