Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/697
Title: uchanganuzi wa lugha ya amani na maridhiano katika muziki nchini kenya (2008-2012)
Authors: MATARA PHILIP NDEMO
Keywords: MUZIKI
LUGHA YA AMANI
Issue Date: 12-Jan-2014
Publisher: MOI UNIVERSITY
Abstract: Utafiti huu ni uchanganuzi wa lugha ya amani na maridhiano katika muziki nchini Kenya (2008-2012). Ulilenga kuchanganua matumizi ya kipekee ya lugha na jinsi maudhui ya amani na maridhiano yanavyowasilishwa katika muziki tuliouteua. Utafiti huu ulichanganua upekee katika uteuzi wa maneno, vishazi na sentensi kwa kuzingatia uhusiano wa vipengele hivi kiwima na kimlalo. Unatanguliza kwa kueleza misingi ya utafiti na uamilifu wa muziki kisiasa, kiuchumi na kijamii. Aidha, umeangazia matumizi ya kipekee ya lugha katika uwasilishaji wa ujumbe wa amani na maridhiano jinsi maudhui ya amani na maridhiano yameumbwa na kuwasilishwa ndani ya jumbe anuwai kwenye muziki ulioteuliwa. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kubainisha muziki uliotumiwa kuendeleza amani na maridhiano nchini Kenya kati ya mwaka wa 2008 na 2012, kupambanua matumizi ya kipekee ya lugha katika ubunaji wa wanamuziki kwa kuzingatia maneno, vishazi na sentensi na kufafanua ujumbe katika muziki wa amani na maridhiano katika muziki nchini Kenya (2008-2012). Nadharia ya majukumu ya lugha ya Halliday pamoja na mawazo ya Fairclough kuhusu uchanganuzi makinifu wa diskosi yalitoa msingi wa kinadharia kwa utafiti huu. Uamilifu anuwai wa muziki katika kuwasilisha maudhui ya amani na maridhiano umeangaziwa kwa kuuhusisha na majukumu ya lugha. Ufasiri wa uteuzi wa lugha umechanganuliwa kwa kuzingatia mawazo kuhusu uchanganuzi makinifu wa diskosi kama mchakato wa kijamii. Data ya utafiti huu iliteuliwa kimakusudi. Nyimbo ishirini zisizo za kidini zilizoimbwa nchini Kenya baina ya mwaka wa 2008 na 2012 zilichunguzwa. Mbinu ya unukuzi wazi ilitumiwa ili kuzalisha data iliyochanganuliwa. Nimetumia maelezo ya kinathari katika kuichanganua data. Utafiti huu ulibainisha kwamba kuna uteuzi wa kipekee wa lugha katika uwasilishaji wa ujumbe wa amani na maridhiano. Aidha, imebainika kuwa uteuzi huu aghalabu unatawaliwa na muktadha ambamo muziki unatungwa na kuchezwa pamoja na uamilifu unaolengwa kutimizwa na wasanii mbalimbali. Isitoshe, kupitia kwa utafiti huu imebainika kwamba lugha huweza kutekeleza majukumu mbalimbali katika jamii. Majukumu haya ni kama vile: kuhimiza amani na maridhiano, kuionya jamii dhidi ya mienendo inayotishia amani na maridhiano pamoja na kutoa wasia wa jinsi ya kuhakikisha kwamba jamii inapata amani ya kudumu miongoni mwa majukumu mengine. Utafiti huu ni mchango katika kuelewa jinsi lugha inaweza kutumika kwa namna chanya ili kuleta maendeleo katika jamii. Utafiti unapendekeza kutambuliwa na kupanuliwa kwa uamilifu wa muziki katika kuzungumzia masuala muhimu yanayoikabili jamii.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/697
Appears in Collections:School of Education

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
tasnifu.pdf962.93 kBAdobe PDFThumbnail
View/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.