Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/6810
Title: Mwingilianotanzu na uchimuzi wa maudhui katika fasihi bunilizi za watoto
Authors: Kirui, Cherono C.
Keywords: Bunilizi
Issue Date: 2022
Publisher: Moi University
Abstract: Japo bunilizi nyingi za watoto katika fasihi ya Kiswahili zinabainisha sifa za mwingilianotanzu kiumbo, hakuna utafiti ambao umeangazia suala hili. Utafiti huu unachunguza namna mwingilianotanzu unachimuza maudhui katika fasihi bunilizi za watoto. Malengo ya utafiti huu ni mosi; kupambanua namna tanzu mahsusi zinajenga bunilizi teule za watoto. Pili, kuchanganua namna tanzu mahususi zinachimuza maudhui katika bunilizi teule za watoto na tatu ni kuhakiki uamilifu wa maudhui kwenye tanzu husika kwa mtoto Mwafrika katika mazingira yake. Ili kutimiza malengo haya, utafiti uliongozwa na maswali yafuatayo: Kwanza, ni tanzu zipi zinazojenga fasihi bunilizi za watoto wa daraja la tatu? Pili, ni kwa namna gani vipengele vya mwingilianotanzu vinachimuza maudhui katika fasihi bunilizi teule za watoto? Mwisho, tanzu na maudhui yanayowasilishwa kwa bunilizi teule yana uamilifu upi kwa mtoto Mwafrika? Utafiti huu umejikita katika vitabu teule vya watoto; Mchezo wa Mtelezo na Hadithi Nyingine (Nandwa, 2016), Kade na Katana (Syokau, 2018), Mchezo wa Kobole (Momanyi, 2019), Kito Apepeta (Nandwa, 2013), Sitaki Iwe Siri (Matundura, 2008), Hidaya (Namlola, 2019), na Msiba wa Kujitakia (Kea, 2013). Nadharia ya Mwingilianomatini yake Kristeva (1960) na Nadharia ya Uoniafrika ya Asante (1980) ndizo kiunzi cha utafiti huu. Kristeva (1960) anadai kuwa matini siku zote huingiliana na kutegemeana. Ni kwa msingi huu ndipo utafiti huu unachunguza namna tanzu anuwai zinaingiliana na kuchimuza maudhui katika bunilizi teule za watoto. Kwa upande mwingine, Uoniafrika unasisitiza kuwa maisha ya Mwafrika lazima yatathminiwe kwa kuzingatia mwonoulimwengu wake. Nadharia hii ilituongoza kuhakiki namna tanzu zinazoingiliana katika bunilizi teule zinamwangazia mtoto Mwafrika katika mazingira yake. Ukusanyaji wa data ya kimsingi ulitokana na bunilizi saba za watoto. Sampuli ya kimakusudi ilitumiwa kuteua bunilizi hizo. Data ilichanganuliwa kiufafanuzi kulingana na maswali ya utafiti na mihimili ya nadharia za utafiti. Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kuwa mwingilianotanzu ni mojawapo ya mbinu ya kisanaa inayochimuza maudhui kama vile umaskini, dini, uzalendo, utangamano na mengine katika bunilizi teule. Utafiti huu ni kichocheo kwa wahakiki wa fasihi ya Kiswahili kuchunguza namna mwingilianotanzu unachimuza maudhui katika tanzu nyinginezo za fasihi andishi na simulizi. Aidha, utafiti huu unachangia pakubwa katika kubainisha vigezo vya utunzi hasa wa fasihi ya watoto katika Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/6810
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
CHERONO KIRUI TASNIFU.pdf1.75 MBAdobe PDFView/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.