Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/4903
Title: Uhakiki wa sitiari na tasfida katika mawasiliano kuhusu vvu/ukimwi miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu: kifani cha chuo kikuu cha Moi
Authors: Momanyi, Lilian
Keywords: sitiari
UKIMWI
tasfida
Issue Date: 2021
Publisher: Moi University
Abstract: Utafiti huu ulichunguza sitiari na tasfida katika mawasiliano kuhusu VVU/UKIMWI miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kujikita kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Moi nchini Kenya. Tangu kisa cha kwanza cha Virusi Vinavyosababisha UKIMWI kugunduliwa nchini Kenya 1984, suala la UKIMWI limejitokeza kuwa mada muhimu ya utafiti katika taaluma mbalimbali. Hata hivyo, tafiti zinazohusu tasfida na sitiari zinavyojitokeza katika mawasiliano ya VVU/UKIMWI. Hata hivyo, hakujatokea utafiti makinifu katika tafiti za Kiswahili kuhusiana na matumizi haya ya stiari na tasfida.. Mawasiliano ni hatua muhimu katika mazungumzo yanayohusu VVU/UKIMWI na masuala husika. Hivyo basi, ili kufanikisha mawasiliano, ni muhimu kushughulikia vipengele vinavyotumiwa katika mawasiliano kwa lengo la kutathmini kama vinafanikisha mawasiliano au vinachangia katika kushutumu waathiriwa zaidi. Hili ndilo pengo ambalo utafiti huu ulilenga kuziba. Malengo yaliyoongoza utafiti huu ni pamoja na: kutambua sitiari zilizotumiwa katika mawasiliano yanayohusu VVU/UKIMWI na masuala husika, kubainisha tasfida zilizotumiwa katika mawasiliano ya VVU/UKIMWI na masuala husika; na jukumu lililotekelezwa na sitiara na tasfida za Kiswahili kama njia ya mawasiliano na kampeni dhidi ya VVU/UKIMWI. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Umaanisho ya Grice na vilevile nadharia ya Mawasiliano ya Kiutambulisho ya Giles. Msingi wa nadharia ya Giles unaipalilia kauli kwamba watu hufanya marekebisho katika mitindo yao ya usemi kadri wanavyowasiliana na wenzao. Nadharia hii pia inaichukulia lugha kama tukio la utendaji wa kijamii. Nadharia ya Grice nayo inaeleza tofauti za kiutambuzi baina ya kile kinachosemwa moja kwa moja katika sentensi na kile ambacho kinadokezwa tu katika usemi wa maneno maalum. Kuambatana na malengo ya utafiti huu, Chuo Kikuu cha Moi kiliteuliwa kimakusudi kama eneo la utafiti. Uamuzi huu ulitokana na hoja kwamba eneo hili lina wingi wa data iliyotumiwa na kuchanganuliwa katika utafiti huu. Mtafiti alitumia uchunguzi kifani kama muundo wa utafiti ili kuruhusu uchunguzi wa kina zaidi. Uteuzi wa sampuli kiuelekezano na mbinu ya kimakusudi ya uteuzi wa sampuli zilitumiwa kuwateua wasailiwa kutoka kwa sampuli nzima kuambatana na malengo maalum ya utafiti huu. Waliolengwa katika utafiti huu walikuwa vijana ambao wamo kati ya umri wa miaka kumi na nane na miaka thelathini na nane. Utafiti ulitumia mwongozo wa kuendesha mahojiano na hojaji katika kukusanya data ya utafiti. Data iliyokusanywa ilijumuisha vipengele vya kileksia na kauli kamilifu kama zilivyotumiwa katika maingiliano yanayohusu VVU/UKIMWI. Data ilichanganuliwa kwa msingi wa nadharia ya Umaanisho ya Grice na nadharia ya Mawasiliano ya Kiutambuisho ya Giles. Matokeo ya utafiti yaliashiria kwamba wanafunzi wengi walitumia tasfida na kauli za kisitiari kuwasiliana masuala yanayohusu VVU/UKIMWI miongoni mwa vijana katika Chuo Kikuu cha Moi. Isitoshe, mahusiano ya kijamii miongoni mwa vijana yanatekeleza dhima muhimu kama mbinu ya mawasiliano katika jamii. Utafiti vilevile ulibainisha kwamba maana iliyokusudiwa katika kauli za kisitiari pakubwa hueleweka katika msingi wa uamali. Utafiti huu ulihitimisha kwamba wanafunzi wengi huwasilisha ujumbe waliokusudiwa kupitia kwa mbinu za tasfida na sitiari kuambatana na matarajio ya jamii kuhusu adabu katika matumizi ya lugha, ikiwemo kutumia maumbo ya lugha ambayo hayaudhi na yanayokuza maingiliano mazuri ya kimawasiliano miongoni mwa wanajamii. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa muhimu kwa makundi kadhaa ikiwemo wanafunzi wa Kiswahili, Wanaisimujamii, Wachanganuzi wa Diskosi na semi, na watafiti wengine ambao wana ari ya kuchunguza matumizi ya lugha katika mazingira asilia. Utafiti huu ni mchango muhimu kwa kongoo iliyopo tayari kuhusu sitiari na tasfida katika isimu na katika fasihi. Utafiti unapendekeza kwamba tafiti za baadaye zinapaswa kupanua upeo wa uchunguzi kwa kuangazia fani zingine za fasihi na isimu. Aidha, tunapendekeza kwamba watafiti wa baadaye wachunguze mielekeo mingine ya kinadharia katika kuchunguza data pamoja na masuala yaliyoibuliwa.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/4903
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
Lilian Momanyi Thesis.pdf844.69 kBAdobe PDFView/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.