Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/4638
Title: Mviga wa maridhiano katika jamii ya Wanandi: uchunguzi wa Kiuamilifu
Authors: Biwott, Anthony Kipkoech
Keywords: Mviga
maridhiano
Issue Date: 2021
Citation: Moi University
Abstract: Mviga ni mchakato wa kiutamaduni unaohusisha matambiko yanayotekelezwa kupitia kwa ibada maalum. Utafiti huu ulichunguza mviga wa maridhiano miongoni mwa jamii ya Wanandi kama kipera cha utanzu wa maigizo katika fasihi simulizi. Utafiti huu ulilenga kubainisha mchakato wa mviga huo kama kipera cha utanzu wa maigizo katika fasihi simulizi, ukachunguza uamilifu wake katika jamii ya Wanandi na kutathmini nafasi yake katika kusuluhisha migogoro katika karne ya ishirini na moja. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza mchakato wote wa mviga wa maridhiano kama kipera cha fasihi simulizi katika jamii ya Wanandi, kubainisha utendaji wake, na kutathmini nafasi yake katika katika karne ya 21 miongoni mwa Wanandi. Utafiti huu uliendeshwa katika tarafa ya Kipkaren na Kabiyet katika kaunti ya Nandi. Mbinu ya usampuli wa kimakusudi na elekezi ilitumika katika kuteua wasailiwa. Uteuzi wa wasailiwa uliongozwa na sampuli elekezi na ya kimakusudi. Data ilikusanywa kwa kutumia hojaji, utazamaji shiriki, na mahojiano kuhusu mviga wa maridhiano ambayo yalirekodiwa kwa kutumia vinasa sauti na mengine kunakiliwa kwa kutumia kalamu na karatasi. Data iliyokusanywa ilinukuliwa na kutafsiriwa kutoka kwa lugha ya Kinandi hadi Kiswahili, ikasimbwa na kuchanganuliwa kimaelezo kwa kuongozwa na nadharia ya uamilifu kama ilivyopambanuliwa na Radcliff-Brown (1930) ambayo ilituwezesha kuchanganua mchakato wa mviga wa maridhiano na nafasi ya mviga huu katika karne ya 21. Vile vile, nadharia ya utendaji kwa mujibu wa Foley (1995) ilituongoza kubainisha utendaji katika utekelezaji wa mviga wa maridhiano. Utafiti huu ulidhihirisha kwamba katika utekelezaji wa mviga wa maridhiano kama kipera cha fasihi simulizi, mchakato maalum wa kihatua hufuatwa. Aidha, katika utekelezaji wake kuna utendaji unaohusisha matendo mbalimbali, uimbaji, na hata kuboboja maneno. Pia ilibainika kwamba unatumika kuwapatanisha wanajamii, kutakasa, kutahadharisha, kutoa mafunzo na kusisitiza ushirikiano. Vile vile, ilibainika kwamba, katika karne ya 21, hatua za utekelezaji wa mviga huu zingali zinazingatiwa japo baadhi ya vyombo vya utekelezaji wake vimebadilika. Tasnifu hii inapendekeza kuwa tafiti zaidi zifanywe katika kipera hiki cha mviga wa maridhiano katika jamii nyingine k.v. jamii ya Waluhya na Wajaluo. Vile vile, tafiti zifanywe kuhusu aina nyinginezo za miviga k.v. mviga wa kutawaza kiongozi, harusi, mviga wa matanga/mazishi, mviga wa kumpa mtoto jina n.k. Aidha, mwelekeo tulioutumia unaweza ukatumiwa kuchunguza tanzu na vipera vingine vya fasihi simulizi k.v. ngomezi, visasili, masimulizi, vitendawili, methali, nyimbo miongoni mwa nyinginezo.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/4638
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
There are no files associated with this item.


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.