Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/4415
Title: Uhakiki wa makosa katika maandishi ya wanafunzi wa Shule za Upili na baadhi ya vitabu vya Kiada Wanavyotumia Shuleni
Authors: Wafula, Enos Barasa
Keywords: Uhakiki
vitabu vya Kiada
maandishi
Issue Date: 2021
Publisher: Moi University
Abstract: Ukiukaji wa kanuni za kitahajia na kisarufi katika lugha husababisha makosa. Makosa yanayofanywa na wanafunzi wa shule husababisha matokeo duni katika mitihani. Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) hutathmini watahiniwa katika kiwango cha Elimu ya Msingi na Kiswahili ni kati ya masomo ya lazima yanayotahiniwa katika kiwango hiki. Katika siku za hivi karibuni, hasa kati ya 2016 na 2018, utendaji wa wanafunzi katika somo la Kiswahili umekuwa ukizorota na makosa ya kitahajia na kisarufi ni sababu mojawapo ya kudorora huku. Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa kuhakiki makosa katika maandishi ya wanafunzi wa shule za upili katika kaunti ndogo ya Likuyani, kaunti ya Kakamega na katika baadhi ya vitabu vya kiada vya Kiswahili. Malengo mahsusi yalikuwa ni kutambua na kuchanganua makosa ya kitahajia na kisarufi katika maandishi ya wanafunzi na vitabu vya kiada. Tuliongozwa na nadharia tete kwamba makosa katika maandishi na vitabu vya kiada hujidhihirisha kwa namna mbalimbali na kwamba makosa kwenye maandishi ya kiada huigwa na wanafunzi. Tuliongozwa na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa iliyofasiliwa na S. P. Corder. Utafiti huu ulifanywa nyanjani na maktabani ambapo tulizuru Shule tisa za Upili katika eneo la utafiti na kusoma vitabu vitatu vya kiada maktabani. Mazoezi matatu ya kuandika yenye Viasho, Jozi za Mlinganuo Finyu na Insha, yalitumiwa ili kupata data ya uchanganuzi. Kwa kufanya utafiti maktabani, tulipata data ya makosa katika vitabu vya kiada. Data ilichanganuliwa kwa kuzingatia utukiaji wake chini ya vipengele vya udondoshaji, uchopekaji na ubadilishaji wa herufi na maneno. Aidha, tulizingatia utenganishaji na uunganishaji wa maneno katika kitengo cha makosa ya kitahajia. Upatanisho wa kisarufi, minyambuliko na uambishaji ni vipengele vingine tulivyozingatia katika kuchanganua data kuhusu makosa ya kisarufi. Matokeo ya utafiti yalidhihirisha kwamba wanafunzi walifanya makosa yanayofanana na makosa yanayopatikana kwenye vitabu vya kiada. Makosa mengine yalitokana na athari za lugha ya kwanza ya wanafunzi. Tunapendekeza kwamba kadiri tunavyojitahidi kukabiliana na athari za lugha ya kwanza kama sababu kuu ya makosa katika Kiswahili, ni sharti kuwe na umakinifu katika uandishi wa vitabu vya kiada kwani makosa yanapokuwamo, huwa na athari hasi kwa wanafunzi. Kushughulikiwa kwa visababishi hivi kutapunguza makosa ya wanafunzi na kuimarisha utendaji wa wanafunzi katika mitihani ya Kiswahili.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/4415
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
Wafula, Enos Barasa.pdf1.38 MBAdobe PDFView/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.