Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/2350
Title: Usawiri wa mwanamke katika ndoa: mifano kutoka utendi wa Mwanakupona, utendi wa Ayubu na Matini teule za kidini
Authors: Sawe Angela
Keywords: Usawiri
Mwanamke
Ndoa
Issue Date: Oct-2018
Publisher: Moi University
Abstract: Utafiti huu unahusu usawiri wa mwanamke katika kazi teule za fasihi na jinsi maandiko ya kidini yanavyomwangalia mwanamke katika jamii. Kazi hizi teule za fasihi ni Utendi wa Mwanakupona (1858), Utendi wa Ayubu (1723) na maandiko ya kidini ya ‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’ katika Biblia Takatifu, Agano la kale (1921). Katika utafiti huu, tumelinganisha mwanamke anavyosawiriwa katika kazi hizi mbili za fasihi na maandiko matakatifu yanavyotarajia tabia na uhusiano wa mwanamke na mwanamume katika ndoa. Waandishi wengi kwa kuathiriwa na Ufeministi na usawa wa kijinsia, wamemsawiri mwanamke aliyedhalilishwa na kunyanyaswa katika ndoa. Katika utafiti wetu, tumechunguza miongozo inayotolewa katika tendi hizi na kulinganisha na mwongozo wa kidini unaotolewa kupitia ‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’. Mwanamke anaposimamia nafasi yake katika ndoa sio ukandamizaji bali utekelezaji wa majukumu yake katika ndoa. Kwa hivyo, tumechunguza iwapo yapo manufaa katika Utendi wa Mwanakupona, Utendi wa Ayubu, ‘‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’’ katika kukuza na kuujenga uhusiano madhubuti katika ndoa. Ili kuendeleza utafiti huu, tuliteua sampuli ya kimakusudi iliyoafikiana na malengo yaliyoongoza utafiti huu. Malengo kwenye tasnifu hii ni kuchanganua taswira ya mwanamke kutoka kazi hizi teule za fasihi na matini za dini, kutathmini uhusiano wa mwanamke na mwanamume katika Utendi wa Mwanakupona, Utendi wa Ayubu, ‘‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’’, na kubainisha dini kama kigezo muhimu katika uthabiti wa ndoa. Maktabani, utafiti huu ulipata data katika kazi teule za Utendi wa Mwanakupona, Utendi wa Ayubu, ‘Kitabu cha Methali na Wimbo Ulio Bora’. Data hii ilichanganuliwa kwa kutumia takwimu fafanuzi. Fasiri na mitazamo mbalimbali imetolewa na waandishi wengi kuhusiana na kazi zetu tulizozichagua na kuhitimisha kuwa mwanamke amekandamizwa na kudhalilishwa. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Ufeministi na nadharia ya Udenguzi. Nadharia ya Ufeministi huangazia jinsi mwanamke amenyanyaswa katika jamii na mbinu zinazoweza kumkomboa. Nadharia ya Udenguzi inadai kuwa kila tamko lina sura mbili, sura iliyopo na sura ya kupangua wakati ule ule mmoja. Mahitimisho ya utafiti huu ni kuwa mwanamke ana nafasi yake maalum katika jamii kama mpenda amani, kielelezo bora kwa watoto na familia kwa jumla. Utafiti huu vile vile ulibainisha mihimili muhimu inayojenga familia kama vile kusameheana, kufurahishana n.k na kwamba mwanamke na mwanamume wanastahili kuishi pamoja licha ya changamoto na matatizo ya maisha. Ilibainika wazi kuwa Mungu ndiye mwanzilishi wa familia na angependa waliooana waishi kwa amani, na kwa hivyo dini ni kigezo muhimu katika ndoa. Kwa jumla, utafiti huu una mchango mkubwa katika taaluma ya Kiswahili na jamii. Katika utafiti huu tumeonyesha kwamba wosia katika Utendi wa Mwanakupona, taswira ya mwanamke katika Utendi wa Ayubu na matini ya kidini si ukandamizaji wa mwanamke bali ni njia ya kuujenga uhusiano mwema katika ndoa. Wafuasi wa dini hizi mbili wakiyazingatia maelekezo kutoka kwa kazi hizi, basi itakuwa ni mchango mkubwa katika kuimarisha ndoa. Aidha, umechangia katika fasihi ya Kiswahili, Waswahili kama jamii na jamii nyingine duniani, wasomaji na wahakiki wa fasihi ya karne hii, kuziangalia kazi hizi upya, na kwamba zina wosia bora zikijikita katika misingi ya kidini katika ndoa za leo.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/2350
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
ANGELA SAWE THESIS.pdf1.27 MBAdobe PDFThumbnail
View/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.