Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/2346
Title: Uchanganuzi wa upole katika mazungumzo ya vipindi vya Sobetab Kapchi katika idhaa ya KASS FM
Authors: Ngisirei Muge Tecla C.
Keywords: KASS FM
Upole
Radio
Issue Date: Nov-2018
Publisher: Moi University
Abstract: Utafiti huu ulilenga kushughulikia umuhimu wa upole katika mazungumzo kwa kuchanganua mikakati ya upole inayotumika katika vipindi vya Sobetab Kapchi (Maisha ya Jamii) kwenye idhaa ya KASS FM. Ili kutekeleza jukumu hilo, utafiti uliongozwa na madhumuni yafuatayo: kuchanganua mikakati ya upole inayotumika kuwasilisha vipindi vya Sobetap Kapchi (SK) katika idhaa ya KASS FM, kuhakiki athari za uzingatiaji na ukiukaji wa kanuni za upole kwenye vipindi vya SK, kutathmini hali zinazoathiri uteuzi wa mikakati ya upole katika vipindi husika vya SK na kupambanua na kujadili changamoto zinazosawiriwa na wahusika wa mazungumzo ya SK wakati wa utekelezaji wa kanuni za upole. Aidha, utafiti uliongozwa na maswali manne. Kwanza, je, ni mikakati gani ya upole inatumika kuendeleza mazungumzo ya SK kwenye idhaa ya KASS FM? Pili, uzingatiaji au ukiukaji wa mikakati ya upole una athari gani kwa mazungumzo ya vipindi vya SK? Tatu, Ni hali zipi zinaathiri uteuzi wa mikakati ya upole katika mazungumzo ya vipindi vya SK kwenye idhaa ya KASS FM? Mwisho, wahusika wa mazungumzo ya SK wanasawiri changamoto zipi wakati wa kutekeleza mikakati ya upole? Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Upole, hasa mhimili wa ‘kuokoa uso’, kama ilivyopendekezwa na Brown na Levinson. Kulingana na waasisi wa nadharia hii, uso ni thamani ya kijamii ambayo mtu hujipa kulingana na atakavyo kuchukuliwa na wengine. Unarejelea kile ambacho mtu anatamani katika mawasiliano yoyote. Nadharia ya Upole inaeleza kuwa mtu ana aina mbili za uso; uso chanya na uso hasi. Aidha, nadharia hii inasisitiza kuwa mawasiliano yoyote hufanikiwa iwapo washiriki wa mazungumzo wanazingatia kanuni za upole kwa makusudi ya kuokoa nyuso zao na za wenzao. Isitoshe, kila mshiriki wa mazungumzo anatakiwa kuhisi kukubalika na kupewa uhuru wa kutoingiliwa. Sampuli ya utafiti iliteuliwa kimakusudi kuambatana na nadharia ya utafiti, malengo na maswali ya utafiti pamoja na upeo wa utafiti kwa kuangazia masuala mahsusi ya kipindi hiki kulingana na utamaduni wa jamii ya Kikalenjin. ‘Pasta’ Edward Rotich na mwelekezi wa vipindi Winny Jepkorir (‘Koriryo’), ni wahusika wakuu na pamoja nao ni mashabiki waliochangia katika vipindi husika. Vipindi vya SK vilisikilizwa kwa makini kabla ya kunaswa. Kinasa sauti kilitumika kukusanya data kwa kurekodi vipindi vinane vya SK. Mwisho, hoja zinazohusiana na upole zilinakiliwa na kuwekwa kwenye makundi manne ya mikakati ya upole ili kuchanganuliwa. Makundi hayo ni ya mkakati wa kuwa kwenye rekodi, mkakati wa upole chanya, mkakati wa upole hasi na mkakati wa kuwa nje ya rekodi. Uchanganuzi wa data ulifanywa kimaelezo kwa kutumia mazungumzo ya washiriki kama mifano halisi. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa wahusika wa mazungumzo ya SK hutumia mikakati anuwai ya upole kuwasiliana ili kudumisha mahusiano kati yao. Pia, wahusika hao hukumbana na changamoto nyingi wanapotekeleza mikakati ya upole wakati wa mazungumzo. Kutokana na matokeo hayo, utafiti huu ni matini muhimu katika uwanja wa mawasiliano kwenye vyombo vya habari hasa vya redio.Utafiti huu ni mchango mkubwa kwa taaluma ya isimu, hasa kwa wale walimu na wanafunzi wa uamali na isimu-jamii, wanaotafitia suala la upole katika mazungumzo kwenye vyombo vya habari katika lugha yoyote ya Kiafrika, hasa lahaja za Kikalenjin. Pendekezo la jumla ni kuwa watafiti wajitokeze kushughulikia masuala ya upole katika nyanja za fasihi na tafsiri.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/2346
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
Muge Ngisirei T. C..pdf2.34 MBAdobe PDFThumbnail
View/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.