Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/2335
Title: Uleksikalishaji, ukriolishaji na mikakati ya kiwingi- lugha katika diskosi za Sheng’
Authors: Ibala Harriet Khatenje
Keywords: Uleksikalishaji
Ukriolishaji
Kiwingi-lugha
Sheng’
Issue Date: Nov-2018
Publisher: Moi University
Abstract: Utafiti huu ulichunguza uleksikalishaji, ukriolishaji na mikakati ya kiwingi-lugha ambayo hutumika katika ubadilishaji msimbo baina ya Sheng’ na Kiswahili. Madhumuni ya utafiti yalikuwa kuhakiki mbinu za uleksikalishaji zinazotumiwa katika Sheng’ kwa kuzingatia vigezo vya Pegitosca, kufafanua sifa zinazopinga upijini na ukriolishaji wa Sheng’, kupambanua mikakati ya kiwingi-lugha inayojitokeza katika diskosi zenye Sheng’ na kuchanganua tungo zenye Sheng’ kwa kuzingatia nadharia ya 4M. Utafiti wenyewe ulichunguza mbinu za uleksikalishaji na mikakati ya kiwingi- lugha inayotumiwa katika diskosi zenye Sheng’ ili kudhihirisha iwapo msimbo wa Sheng’ ni msimu, lahaja ya Kiswahili, lugha, sajili, Pijini au Krioli. Nadharia mbili zilitumiwa katika utafiti huu: Kwanza, nadharia ya Pegitosca ya Kiingi ilitumiwa katika uhakiki wa mbinu za uleksikalishaji zinazotumiwa katika Sheng’ na pili, nadharia ya 4M ya Myers-Scotton ilitumiwa ili kupambanua mikakati ya kiwingi-lugha na kuchanganua tungo zenye Sheng’. Data ya utafiti huu ilikusanywa kutoka kwa Shule tatu za upili zilizoteuliwa kimakusudi. Familia mbili za mitaani na makundi mawili ya vijana wanaoishi mitaani kutoka mitaa miwili katika kaunti ya Kisumu walihojiwa. Ili kuwafikia watafitiwa mahususi mitaani mbinu ya usampulishaji wa bonge-luji ilitumiwa. Kiranja mmoja katika kila shule iliyoteuliwa alitumiwa kupata sampuli ya wanafunzi 120 ambao walipewa karatasi na kuombwa waandike barua kwa marafiki zao wakitumia lugha waipendayo. Vilevile diskosi baina ya wanafunzi hawa zilirekodiwa. Katika sampuli ya familia za mitaani, mtafiti aliwahoji na akarekodi diskosi za vijana na wazazi waliokuwa wakiishi katika mitaa miwili iliyoteuliwa. Matokeo ya utafiti huu yamethibitisha kwamba Sheng’ ni msimu na si lahaja, Pijini, Krioli wala lugha. Mbinu za kipekee za uleksikalishaji zinazotumiwa katika Sheng’, ambazo hazikuwa zimebainishwa katika tafiti za awali kama ufinyaji wa maana na uhamishaji wa maana ziligunduliwa katika uchunguzi huu. Matokeo hayo yameonyesha kwamba mofimu nyingi amilifu zinazotumiwa katika mtagusano baina ya msimbo wa Sheng’ na Kiswahili huwa za Kiswahili. Kuhusiana na mofimu nne (4M) zinazoshiriki katika ujenzi wa miundo ya UM yenye Sheng’, iligunduliwa kwamba Sheng’ hutumia mofimu amilifu za Kiswahili kwa vile haina mofimu zake amilifu. Hata hivyo, Sheng’ ina mofimu chache amilifu ndiposa tasnifu hii ikahitimisha kwamba msimbo wa Sheng’ ungeimarika kiasi cha kuwa na mofimu amilifu nyingi, huenda ingeweza kutumiwa mara nyingi pia kama lugha solo. Tasnifu hii inapendekeza haja ya kustawisha nadharia ya 4M ili iweze kufafanua pia miundo ya lugha mojamoja, na nadharia ya Pegitosca ili itofautishe nguzo za kuchambua msamiati na istilahi.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/2335
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
Harriet K. Ibala 2018.pdf1.72 MBAdobe PDFThumbnail
View/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.