Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/2333
Title: Mwingilianomatini katika ushairi wa Mathias Mnyampala
Authors: Nicholaus Kyamba Anna
Keywords: Ushairi
Mathias Mnyapala
Issue Date: 2018
Publisher: Moi University
Abstract: Ushairi wa Kiswahili una historia ndefu kutokana na dhima yake katika jamii. Ukweli ni kuwa historia hiyo inatokana na watunzi ambao wamechangia maendeleo ya utanzu huu wa kifasihi. Wapo washairi wengi wa Kiswahili waliotunga mashairi katika nyakati tofauti lakini mchango wa kazi zao haujajulikana kikamilifu katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili. Mmojawapo wa washairi waliosahaulika ni Mathias Mnyampala. Azma kuu ya utafiti huu ni kuchunguza na kuchambua ushairi wa Mathias Mnyampala kimwingilianomatini. Utafiti huu umelenga kuchunguza upekee wa tungo za kishairi za Mathias Mnyampala na kuzihakiki mbinu za kifani zilizotumika kuibua maudhui kwa kuzingatia muktadha wa utunzi wake kimwingilianomatini. Malengo ya utafiti huu ni mosi, kupambanua muktadha wa utunzi uliomsukuma mwandishi kutunga kazi teule za ushairi wa Kiswahili. Pili, kuhakiki mbinu za kifani zinavyotumika kuibua maudhui katika kazi teule za ushairi za Mathias Mnyampala. Tatu, kutathmini mchango wa kazi za ushairi za Mathias Mnyampala katika maendeleo ya ushairi wa Kiswahili. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Mwingilianomatini. Mwingilianomatini ni nadharia iliyoasisiwa na Julia Kristeva miaka ya 1960. Nadharia hii inasisitiza kuwa hakuna matini asilia, bali uhai wa matini moja hutegemea matini nyingine tangulizi. Hivyo basi, matini za fasihi hutegemeana katika kukamilisha maana. Ni kwa msingi huu ndipo uhakiki wa mashairi ya Mathias Mnyampala yamechanganuliwa kimwingilianomatini. Kwa kutumia nadharia hii tumebaini kuwa kazi za Mnyampala zinaingiliana, zinakamilishana na kutegemeana na matini nyingine tangulizi. Utafiti huu ni wa maktabani na nyanjani. Kutoka maktabani, data ilikusanywa kutoka kazi teule zilizochapishwa ambazo ni: Diwani ya Mnyampala (1965), Mashairi ya Hekima na Malumbano ya Ushairi (1965) na Ngonjera za UKUTA Na. 1 (1970). Kutokana na mahojiano ya watafitiwa nyanjani tulipata data kuhusu maisha na historia ya Mnyampala pamoja na miswada yake isiyochapishwa ifuatayo: Hazina ya Washairi, Mahadhi ya Kiswahili na Mashairi ya Vidato. Usampulishaji makusudi ulitumika kuteua kazi tatu zisizochapishwa na usampulishaji nasibu ulitumika kuchagua kazi tatu zilizochapishwa. Data zilichambuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo ya kina yaliyohusisha udondozi na ufafanuzi wa mistari, beti na vifungu vya maneno. Uchambuzi huo unadhihirisha mwingilianomatini wa fasihi simulizi na tamaduni za kisasa katika mashairi ya Mathias Mnyampala. Utafiti huu unadhihirisha kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya muktadha wa utunzi, mbinu za kifani na uibuaji wa maudhui ya kazi teule za Mathias Mnyampala. Matokeo ya utafiti ni kwamba, Mathias Mnyampala amechangia pakubwa katika maendeleo ya ushairi wa Kiswahili. Mojawapo ya mchango wake ni kuongozwa na Nadharia ya Kimapokeo katika utunzi wa mashairi yake. Wanamapokeo wanasisitiza upekee wa shairi la Kiswahili kimuundo hasa urari wa vina na mizani. Kwa kutumia nadharia hii, Mathias Mnyampala aliibua mbinu mpya za utunzi mfano mbinu ya mtiririko na msisitizo. Kupitia utafiti huu tumevumbua miswada, barua na nyaraka mbalimbali za kifasihi zilizotungwa na Mathias Mnyampala zenye mchango mkubwa katika ushairi, fasihi na Kiswahili kwa ujumla. Miswada hiyo ni malighafi ya tafiti za kifasihi na machapisho ya kitaaluma.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/2333
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
KYAMBA ANNA NICHOLAUS.pdf59.26 MBAdobe PDFThumbnail
View/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.