Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/1842
Title: Simulizi za virusi vya Ukimwi/Ukimwi zinavyodhihirika katika nyimbo za jamii za Kenya kibaadausasa
Authors: Alexander, Rotich, Kipkemoi
Keywords: virusi vya Ukimwi
nyimbo
Jamii
Issue Date: Sep-2018
Publisher: Moi University
Abstract: Ni zaidi ya miaka thelathini tangu janga la Virusi Vya Ukimwi/ UKIMWI almaarufu VVU/UKIMWI liibuke na kusababisha madhara si haba kwa wanajamii kote ulimwenguni. Serikali za mataifa kote ulimwenguni zimeweka mikakati mbalimbali inayolenga kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu ambao mpaka sasa hauna tiba. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza mchango wa nyimbo za Kiasili na za Kiswahili katika vita dhidi ya VVU/UKIMWI. Utafiti ulilenga kuchanganua nyimbo husika ili kubainisha namna wanajamii wanavyozitumia lugha kiuimbaji katika kulijadili suala hili huku ukibainisha mtazamo wao kuhusu ugonjwa huu. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Baadausasa hasa mawazo ya Michel Foucault katika kuhakiki jinsi miundo na taratibu za kijamii zilivyowezesha asasi kuwa na mamlaka na udhibiti kwa kuwatenga wanajamii wengine hasa wendawazimu, wangonjwa, wachochole, wahalifu na waliokiuka maadili. Anahoji kuwa, daima diskosi haiwezi kutenganishwa na mamlaka kwa sababu ndicho kinachotawala na kuamuru au kuongoza njia za mawasiliano za kila taasisi. Huamua kile kinachoweza kusemwa, vigezo vya ‘ukweli’, nani ana mamlaka ya kusema na ni wapi usemi wa aina hiyo unaweza kutokea. Kwa kuongozwa na mtazamo huu utafiti huu ulichanganua simulizi kuu na simulizi ndogo za VVU/UKIMWI zilizomo kwenye nyimbo kwa kubainisha namna zinavyoweza kupinga ukiukaji wa maadili, kutoa maonyo na faraja pamoja na kukuza au kuudumaza unyanyapaa. Data zilizokusanywa kwa kutumia mbinu za utazamaji, mijadala ya makundi teule na usaili wa ana kwa ana kisha kuripotiwa katika tasnifu hii zilitokana na kazi zawasanii walioteuliwapamojana vituo vya utangazaji. Nyimbo ishirini na tatu ziliteuliwa kimakusudi. Nyimbo kumi na tatu zilikuwa za Kiswahili, nne zilikuwa za Kikalenjin, nne zilikuwa za Kijaluo na mbili zikiwa za Kimaasai. Mtafiti alizitafsiri nyimbo za Kikalenjin kwa kuwa yeye ni msemaji wa lugha husika.Aidha, mbinu ya sampuli kimaksudi ilitumiwa kuwateua wasemaji wa Kimaasai na Kijaluo ili kutafsiri nyimbo kutoka jamii husika. Mbinu za uchanganuzi zilihusisha maelezo na ufafanuzi. Matokea ya utafiti huu ni kwamba, nyimbo katika muktadha wa baadausasa zina simulizi kuu na simulizi ndogo zinazolenga kujadili suala la VVU/UKIMWI. Aidha utafiti ulibainisha jinsi nyimbo zinavyoweza kupindua nguvu za awali au zilizokuwa zinatawala kama zile za kisayansi na wanajamii kuhusu VVU/UKIMWI na waathiriwa. Utafiti huu unachangia tafiti zilizotangulia hasa ikizingatiwa kuwa, nyimbo zinaweza kuwa njia mbadala inayoweza kutumiwa kukabiliana na janga la UKIMWI. Ni rai ya utafiti kwamba jamii imehodhi simulizi sadifu za ugonjwa huu kwani waimbaji wana njia zao mahususi za kuujadili. Kwa kuwa mbinu za kisayansi hazijafaulu kabisa katika vita dhidi ya VVU/UKIMWI, kuna haja ya kutumia mbinu anuwai zikiwemo za kitamaduni kama vile nyimbo pamoja na mbinu za kisayansi. Kutokana na utafiti huu, inapendekezwa kwamba, tafiti zaidi zifanywe katika nyimbo za jamii nyingine pamoja na katika vipera vingine vya fasihi simulizi ili kubainisha simulizi za VVU/UKIMWI zilizomo pamoja na umuhimu wake katika vita dhidi yake.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/1842
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
SASS-DPHIL-KIS-01-10.pdf1.34 MBAdobe PDFThumbnail
View/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.