Please use this identifier to cite or link to this item:
http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/10187| Title: | Uchanganuzi kimtindo wa masuala ya dini na mamlaka katika riwaya teule za kiswahili |
| Authors: | Kyomuhendo, Victor |
| Keywords: | Riwaya Mamlaka |
| Issue Date: | 2025 |
| Publisher: | Moi University |
| Abstract: | Utafiti huu unachunguza nduni mahsusi za kimtindo zinazotumiwa na waandishi wa riwaya teule za Kiswahili kusawiri maudhui ya dini na mamlaka. Riwaya zilizoteuliwa ni: Paradiso (2005) ya John Hamu Habwe, Nguvu ya Sala (1999) ya Kyallo Wadi Wamitila , Asali Chungu (1978) ya Said Ahmed Mohamed, pamoja na Kasri ya Mwinyi Fuad (1978) ya Shafi Adam Shafi. Ingawa kijuujuu riwaya hizi zinachunguza maudhui ya dini na mamlaka, kiundani zinachunguza masuala kama vile jinsia, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, uhalifu mijini, umaskini, ufisadi, tamaa ya pesa na mali, na ukandamizaji. Haya ni masuala ibuka ambayo waandishi wa riwaya teule wanayaangazia kwa mtazamo wa dini na mamlaka. Mkabala wa kimtindo haujatumika sana kuchunguza masuala ibuka kama haya katika riwaya ya Kiswahili. Uchunguzi huu uliongozwa na malengo yafuatayo: kufafanua jinsi uteuzi wa kileksika unavyojitokeza kama nduni ya kimtindo katika kuchimuza masuala ya dini na mamlaka katika riwaya teule. Kuchanganua matumizi ya nduni za kisintaksia katika kuchimuza maudhui ya dini na mamlaka katika riwaya teule. Kuhakiki matumizi ya tamathali za usemi kama mbinu za kimtindo katika uchimuzi wa masuala ya dini na mamlaka katika riwaya teule. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Uchimuzi. Uchanganuzi wa data uliongozwa na mihimili ya Nadharia ya Uchimuzi: ukiushi na usambamba. Utafiti huu ni wa kitaamuli na tulitumia muundo wa usanifu kifani. Mkabala wa kitaamuli ulitumiwa kwa sababu utafiti huu unazingatia fasiri ya ruwaza za nduni mahsusi za kiisimu, mintarafu ya masuala ya dini na mamlaka. Tena, tulizingatia mfumo wa kifalsafa wa kiufasiri. Data ilikusanywa kutoka riwaya nne za Kiswahili ambazo ziliteuliwa kimaksudi. Mahitimisho ya utafiti yaliwasilishwa kidhamira. Kuhusu lengo la kwanza, utafiti huu uligundua kwamba visawe na urudiaji ndiyo mikakati ya kileksika iliyotumiwa zaidi na waandishi kuibua masuala ya dini na mamlaka katika riwaya teule. Kuhusu lengo la pili, iligundulika kwamba anafora na usambamba wa kiusawe ndizo mbinu za kiusambamba zilizotumika zaidi katika riwaya teule. Aina nyingine za usambamba zilizotumiwa ni pamoja na epifora, tanakuzi, na mgeuko wa polepole. Kuhusu lengo la tatu, tamathali ya usemi iliyotumiwa zaidi kuchimuza maudhui ya dini na mamlaka ni sitiari. Hata hivyo, mbinu za tashbihi, kinaya na kejeli pia zilitumika sana katika riwaya zote zilizochanganuliwa. Kwa jumla, inadhihirika kwamba mamlaka yana dhima muhimu sana katika maisha ya wanajamii kwa vile yamefumwa katika mfumo wao wa kijamii, kisiasa, na kiuchumi. Utafiti huu unaonyesha kwamba waandishi wanadhamiria kujenga maudhui kuhusu masuala ya dini na mamlaka na wanatumia mbinu zinazoonyesha jinsi ambavyo matini zinajadili masuala ya muhimu katika jamii zinazosawiriwa. Utafiti huu unasisitiza haja ya kuziangalia matini kama mazao ya jamii husika zinazosawiriwa. Unabainisha utaratibu wa kuzichanganua riwaya za Kiswahili kwa kuzingatia ngazi za kileksika, kisarufi na kisemantiki. Utafiti huu unapendekeza tafiti nyingine za kimtindo zifanywe kwa kuzingatia nadharia nyingine kuchunguza masuala ya dini na mamlaka. Pia akili unde ihusishwe katika utafiti wa kimtindo. |
| URI: | http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/10187 |
| Appears in Collections: | School of Arts and Social Sciences |
Files in This Item:
| File | Description | Size | Format | |
|---|---|---|---|---|
| KYOMUHENDO VICTOR DPHIL-2025.pdf | 1.69 MB | Adobe PDF | View/Open |
Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.