Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/10055
Title: Uhifadhi wa utamaduni kupitia Tafsiri ya Riwaya za Kaburi Bila Msalaba na Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulhawali
Authors: Makini, Georginah Nyatichi
Keywords: Utafiti
riwaya
Issue Date: 2025
Publisher: Moi Univerisity
Abstract: Taaluma ya tafsiri inajumuisha si tu kubadilisha maneno kutoka lugha moja hadi nyingine, bali pia kuhamisha na kutafsiri maadili, desturi na mitazamo mbalimbali ya kitamaduni. Utafiti huu ulikusudia kueleza na kuchanganua jinsi uhifadhi wa utamaduni umeendelezwa kupitia tafsiri ya riwaya za Kaburi Bila Msalaba (Kareithi) na Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali (Kitereza). Utafiti uliongozwa na madhumuni matatu: kubaini vipengele vya kitamaduni katika matini teule, kutoa maelezo yanayothibitisha kwamba riwaya hizi mbili ni hazina ya hifadhi ya utamaduni wa maisha ya jamii mahususi za Kiafrika; kujadili na kuitathimini michakato na mikakati iliyotumiwa kutafsiri kazi chanzi kama mikakati ya uhifadhi wa utamaduni katika riwaya hizi mbili; kuonyesha jinsi udumishwaji wa baadhi ya vipengele vya lugha chanzi (Kiswahili na Kikerewe) unavyoweza kufasiriwa kama ithibati ya uhifadhi wa utamaduni katika tungo asilia na katika tafsiri. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili: nadharia ya anthropolojia na nadharia ya Skopos. Nadharia ya anthropolojia ilizingatia tapo la isimu anthropolojia ambalo linachunguza tabia na mienendo ya watu na jinsi wanavyotumia lugha kwa lengo la kuonyesha ukweli na uhalisia wa mambo katika jamii. Nadharia ya Skopos huchukulia shughuli ya kutafsiri kama kitendo kilicho na malengo. Yaani, kabla mtafsiri hajaanza kazi yake ni sharti aelewe lengo la tafsiri yake. Utafiti ulikuwa wa maktabani. Mtafiti alijikita katika riwaya za Kareithi na Kitereza na tafsiri zao katika lugha ya Kiingereza. Matini teule zilisomwa na data msingi kurekodiwa. Data ilipangwa na ilichanganuliwa kulingana na malengo ya utafiti na matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo. Kuhusu lengo la kwanza, utafiti uligundua kwamba fasihi haiumbwi katika ombwe tupu bali hufungamanishwa na maisha ya binadamu na mazingira yake. Dhana za kitamaduni zinapotafsiriwa huwa ni njia moja ya kuhifadhi utamaduni kwa hadhira lengwa. Mintarafu ya lengo la pili, utafiti ulibaini kwamba mikakati maalum ilitumiwa ili kuhawilisha vipengele vya kitamaduni kutoka matini chanzi hadi hadhira lengwa jinsi nadharia ya Skopos inavyoweka. Vipengele vingi vya kitamaduni katika matini asilia viliweza kudumishwa kupitia mikakati mbalimbali ya tafsiri. Kulingana na lengo la tatu, utafiti ulionyesha kwamba mbinu nyingi za ujielezaji hufungamana na utamaduni na miktadha ya kila siku ya jamii husika. Mbinu hizi zinapohawilishwa mikakati maalum hushirikishwa na hii huwa ni njia moja ya kuhifadhi utamaduni kupitia mchakato wa tafsiri. Utafiti ulihitimisha kwamba uhifadhi wa utamaduni unawezeshwa kupitia mchakato wa tafsiri. Utafiti huu unapendekeza kuwe na tafiti zingine zinazozingatia maandishi ambayo hayakushughulikiwa katika utafiti huu kama vile tamthilia na hadithi fupi. Aidha, utafiti unaweza kufanywa kwa kutumia nadharia tofauti kando na nadharia ya anthropolojia na nadharia ya Skopos.
URI: http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/10055
Appears in Collections:School of Arts and Social Sciences

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
Nyatichi georgina Makinifinal -29-08-2024Lib (2).pdf1.11 MBAdobe PDFView/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.